Jeuri ya fedha kwisha, adhabu ya alama kurejesha heshima Ligi Kuu

Timothy Lugembe,

Mwanakwetusports.

Kwa muda mrefu adhabu ya faini imekuwa njia kuu ya kushughulikia ukiukaji wa kanuni katika Ligi Kuu Tanzania Bara ambapo kwa baadhi ya klabu zenye uwezo wa kifedha, adhabu hiyo haikuonekana kuwa na athari kubwa. Kulipa fedha kulikuwa rahisi kuliko kubadili tabia, hali iliyosababisha baadhi ya makosa kujirudia mara kwa mara na kuacha taswira ambayo haikujenga hadhi ya ligi inayotaka kuwa ya ligi ya kisasa.

Hatua ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kuingiza adhabu ya kukatwa alama tano kwa timu itakayokiuka matumizi ya vyumba rasmi vya kubadilishia nguo ni mwanzo wa mabadiliko yanayolenga kurejesha uzito wa sheria ambapo adhabu ya alama haiathiri tu upande wa fedha, bali kuathiri moja kwa moja ushindani wa timu kwenye msimamo wa ligi na hapo ndipo thamani ya sheria inaanza kuonekana.

Kwa mujibu wa Rais wa TFF, Wallace Karia, uamuzi huo umetokana na matukio yaliyojitokeza msimu uliomalizika 2025/26 , ambapo baadhi ya klabu zilitumia maeneo ambayo hayajatengwa rasmi kama vyumba vya kubadilishia nguo huku miongoni mwa matukio yaliyotajwa ni matumizi ya "Jumba la Maajabu " badala ya vyumba rasmi katika michezo iliyochezwa Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo, ikiwemo michezo ya Yanga dhidi ya Simba na Yanga dhidi ya JKT Tanzania, ambapo klabu ya Yanga ilihusika kwenye sakata hilo.

Kilichotia wasiwasi zaidi si tukio lenyewe, bali namna baadhi ya klabu zilivyoonekana kutokuwa na hofu ya adhabu, Faini ilipoonekana kuwa ndogo ukilinganisha na uwezo wa kifedha wa baadhi ya timu makosa yaliendelea kujitokeza.

Kuna wakati mashabiki waligeuzwa chanzo cha kulipia gharama hizo kupitia michango iliyotolewa baada ya klabu kutangaza namba za malipo kwenye mitandao ya kijamii Mwisho wa siku adhabu iliyokusudiwa kufundisha ilimalizika bila kuleta mabadiliko ya tabia, na tukio la kutoa namba ya malipo ya faini kwa mashabiki ilionekana ni jeuri ya wazi ikitoa mtazamo kuwa kwa vilabu vikubwa adhabu ya fedha kwao sio tatizo.

Kupitia hilo , adhabu ya kukatwa alama inaenda kubadili mwenendo wa jeuri ya kifedha na hakuna timu inayoweza kupuuza kupoteza alama tano katika mbio za ubingwa au mapambano ya kuepuka kushuka daraja ambapo athari yake ni kubwa kuliko faini, hivyo inalazimisha kila mshiriki kuheshimu kanuni bila kujali uwezo wake wa kifedha.

Hatua ya TFF pia ya kuboresha vyumba vya kubadilishia nguo kwa kuvifunga vifaa vya kisasa vya ufuatiliaji inaonyesha kuwa utekelezaji wa sheria utaenda sambamba na uwekezaji katika miundombinu, endapo kutakuwa na malalamiko kuhusu mazingira ya vyumba hivyo, ushahidi utaweza kupatikana kwa urahisi na hatua kuchukuliwa kwa kuzingatia kanuni.

Hivyo, ligi inayotaka kuheshimika ndani na nje ya nchi haiwezi kujengwa kwa sheria zisizotekelezwa, nidhamu ni sehemu ya ushindani, na ushindani hujengwa kwa kufuata taratibu zinazofanana kwa kila mshiriki na Pale ambapo hakuna anayekuwa juu ya sheria, ndipo hadhi ya mashindano huongezeka.

Kwa mtazamo huo, uamuzi wa TFF unastahili kuungwa mkono, chini ya uongozi wa Wallace Karia, shirikisho limeonyesha kuwa wakati umefika wa kuondoka kwenye mfumo ambao adhabu za fedha zilionekana kuwa jambo la kawaida kwa baadhi ya klabu . Ikiwa kanuni hizi zitatekelezwa kwa usawa kwa kila timu, Ligi Kuu Tanzania Bara inaweza kujijengea mazingira yenye nidhamu zaidi, ushindani wa haki na hadhi inayokidhi viwango vya soka la kisasa.

0767915473,

lugembetimothy01@gmail.com.



0/Post a Comment/Comments