BONANZA Kuelekea SHIMIWI 2026 Lafana.

 

Adeladius Makwega

Ofisi ya Rais Idara ya Kumbukumbu na Nyaraka-DODOMA.

 

Asubuhi ya Agosti 15, 2026, Dodoma iligeuka kuwa uwanja wa furaha, ushindani, vifijo, miluzi, mshikamano na shangwe. Watumishi wa umma kutoka taasisi mbalimbali walitoka maofisini na kuingia uwanjani—wakakimbia, wakavuta kamba, wakapiga pasi na kushangilia, yote ikiwa ni sehemu ya maandalizi kuelekea Michezo ya Watumishi wa Umma (SHIMIWI) 2026.

 

Bonanza hilo maalumu halikuwa tu suala la kutafuta mshindi; lilikuwa ni pasi ya kujenga afya, urafiki na timu imara ya watumishi wa umma.

 

Katibu Mkuu Kiongozi, Dkt. Moses Kusiluka, aliipongeza Wizara ya Utumishi na Utawala Bora kwa kuendelea kuhamasisha michezo, akisisitiza kuwa michezo hujenga afya, mahusiano na kuongeza tija kazini.

 

Kwa niaba yake, Katibu Mkuu wa Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Juma Seleiman Mkomi, alimuwakilisha vema kiongozi huyu huku akiseama michezo inawafanya watumishi kujuana zaidi, kujenga mshikamano na kuimarisha ushirikiano katika kutekeleza majukumu ya Serikali.

 

Akisisitiza umuhimu wa michezo huku akishangiliwa na watumishi wa umma, Mkomi aliwataka Wakurugenzi na Maafisa Rasilimali Watu kuhakikisha watumishi wanapatiwa nafasi, vifaa na mazingira rafiki ya kushiriki michezo.

 

Naye Dkt. Kusiluka akataka michezo iwe sehemu ya utamaduni wa taasisi za umma nchini.

 

Uwanjani, Ofisi ya Rais, Idara ya Kumbukumbu na Nyaraka nayo haikubaki benchi. Timu zake ziliingia dimbani katika michezo mbalimbali, ikiwemo soka na kuvuta kamba, zikionesha kuwa maandalizi ya SHIMIWI 2026 yameanza kwa kasi ya moto wa kuotea mbali.

 

Hapa hakuna benchi la akiba—kila mtumishi ni mchezaji, kila mchezo ni mazoezi, na kila mshikamano ni ushindi.

 

Huku Mwanakwetu akijinyakulia rafiki mmoja mrembo kutoka Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo ambaye alibadilishana naye namba jina lake linabaki kuwa siri, kweli bonanza hili limezaa matunda.Wale watumishi wa umma waliokosa bonanza hili wamekula wa chuya.

 

Yote hayo ni ishara ya kipenga chaSafari ya SHIMIWI 2026 imeanza rasmi; kutoka ofisini hadi uwanjani, lengo ni moja: afya, mshikamano, nidhamu na tija katika Utumishi wa Umma.

 

makwadeladius@gmail.com

0717649257












0/Post a Comment/Comments