Timothy Lugembe,
Mwanakwetusports.
Hatima ya mshambuliaji Julian Alvarez imeendelea kuwa suala linaloibua mvutano ndani ya Atletico Madrid, huku Barcelona ikiendelea kuonyesha nia ya kumsajili licha ya msimamo wa klabu kutotaka kumuuza kwenye klabu hiyo.
Alvarez amekuwa akihusishwa na Barcelona tangu mwanzoni mwa dirisha la usajili, huku taarifa zikieleza kuwa mchezaji huyo angependa kuhamia Camp Nou ikiwa ataondoka Atletico . Rais wa Barcelona, Joan Laporta, amesema kuwa klabu hiyo bado inamtaka mshambuliaji huyo na inaendelea kusubiri uwezekano wa makubaliano yakumnasa.
Hata hivyo, Atletico Madrid imeweka msimamo tofauti ambapo uongozi wa klabu hiyo umesema hauna mpango wa kumuuza Alvarez, hasa kwa Barcelona, huku ukisisitiza kuwa mchezaji huyo ana mkataba hadi Juni 2030.
Msimamo huo umejengwa tangu miezi ya nyuma ambapo Atletico iliwahi kukataa ofa ya euro milioni 150 kutoka Real Madrid na kuelekeza klabu hiyo kwenye kipengele cha kuvunja mkataba chenye thamani ya euro milioni 500.
Katika hatua nyingine, uongozi wa Atletico umesema haukubali ofa ya euro milioni 100 na hautakuwa tayari pia kwa euro milioni 150 au milioni 200 kwa mchezaji wao. Hilo limeonyesha kuwa suala hilo si la bei pekee, bali pia linahusisha msimamo wa klabu kuhusu mustakabali wa mshambuliaji huyo.
Mvutano huo umeanza kuonekana pia upande wa mashabiki, wakati ambao mchezaji amekutana na changamoto ya kuzomewa na baadhi ya mashabiki wa Atlético katika mchezo wa hivi karibuni, jambo linaloonyesha jinsi sakata la usajili linavyoanza kuathiri uhusiano kati yake na sehemu ya mashabiki wa klabu hiyo.
Kwa upande wa Barcelona, hitaji la kumnasa mshambuliaji mwingine limeendelea kuwa sehemu ya mipango ya klabu hiyo baada ya mabadiliko katika safu yake ya ushambuliaji huku Alvarez akionekana kuwa miongoni mwa chaguo linalopendwa na uongozi wa Barcelona, lakini Atletico bado haijaonyesha nia ya kufungua mlango wa mazungumzo.
Hali hiyo imefungua pia uwezekano wa klabu nyingine kuingia kwenye kinyang'anyiro na Arsenal imehusishwa na Alvarez katika siku za mwisho za dirisha la usajili, huku Atletico ikiwa na mtazamo wa kusikiliza uwezekano wa ofa kutoka nje ya La Liga kuliko kumruhusu mchezaji huyo kwenda Barcelona.
Alvarez alijiunga na Atletico mwaka 2024 akitokea Manchester City na amekuwa sehemu muhimu ya timu hiyo akiwa amefikisha mabao 49 na asisti 17 katika mechi 107 akiwa na klabu hiyo.
0767915473,
lugembetimothy01@gmail.com.



Post a Comment