Agosti 12 na mwanzo wa enzi mpya ya teknolojia katika soka la Tanzania

Timothy Lugembe,

Mwanakwetusports.

Soka la Tanzania limeanza kutumia teknolojia ya Football Video Support (FVS) katika kusaidia waamuzi kufanya maamuzi kwenye matukio muhimu ya mchezo, Mfumo huo umeanza kutumika kwa mara ya kwanza nchini Agosti 12, 2026, katika mchezo wa Ngao ya Jamii uliowakutanisha Simba na Yanga kwenye u anja wa New Amaan Zanzibar.

Katika mchezo huo, Yanga imeibuka na ushindi wa bao 1-0 na kutwaa Ngao ya Jamii, mbali na matokeo ya mchezo, matumizi ya FVS yalikuwa sehemu nyingine muhimu ya pambano hilo kwa kuwa yaliashiria kuanza kwa matumizi ya mfumo huo katika soka la Tanzania.

FVS ni mfumo unaotumia video kumsaidia mwamuzi pale kunapotokea tukio ambalo linaweza kuwa na uamuzi usio sahihi, tofauti na VAR, FVS haifanyi kazi kwa mfumo wa chumba cha waamuzi wa video wanaofuatilia mchezo muda wote badala yake, kocha anaweza kuomba tukio lipitiwe kwa kutumia video.

Kwa kutumia teknolojia hii, mwamuzi ndiye mwenye uamuzi wa mwisho baada ya kwenda kwenye monitor na kuangalia tukio hivyo, teknolojia hiyo haiondoi mamlaka ya mwamuzi, bali inampa nafasi ya kupata taarifa zaidi kabla ya kuthibitisha au kubadilisha uamuzi wake.

Mfumo huo unaweza kutumika katika matukio kama bao, penalti, kadi nyekundu ya moja kwa moja na utambulisho wa mchezaji anayepaswa kupewa adhabu, hata hivyo, si kila tukio la mchezo linaweza kupelekwa kwenye mapitio ya video.

Katika uendeshaji wake Kila timu hupewa nafasi nne za kuomba marejeo ya matukio yanayo onekana kuwa tata , ikiwa timu itaomba marejeo ya tukio fulani na mwamuzi akipitia akakuta maamuzi yake ya awali ni sahihi basi timu hiyo itapoteza nafasi Moja ya kufanya marejeo , na ikiwa mwamuzi ataitwa kurejea tukio na akakuta alifanya makosa kwenye uamuzi wake basi timu itabaki na nafasi zili zile nne za kuomba marejeo.

Kwa Tanzania, matumizi ya FVS yatasaidia kupunguza malalamiko yanayotokana na maamuzi ya waamuzi, hasa kwenye matukio ambayo yanaweza kuonekana tata na kuleta sintofahamu kwa mwamuzi na benchi la ufundi hapo ndipo Kocha anapokuwa na nafasi ya kuomba mapitio ili kuhakiki uamuzi.

Hata hivyo, FVS haitamaliza kabisa malalamiko dhidi ya waamuzi, mwamuzi bado ndiye anayefanya uamuzi wa mwisho baada ya kutazama video, na baadhi ya matukio ya soka yanahitaji tafsiri ya sheria. Kinachobadilika ni kwamba mwamuzi anapata nafasi ya kuliona tena tukio kabla ya kufanya uamuzi wa mwisho.

Kwa upande wa TFF, kuanza kwa matumizi ya FVS ni hatua katika kuongeza matumizi ya teknolojia kwenye mashindano ya ndani mfumo huo pia unatoa njia ya Tanzania kutumia msaada wa video bila kuingia moja kwa moja kwenye gharama na mahitaji yote ya mfumo kamili wa VAR ambao unatumia gharama kubwa za uendeshaji.

Chini ya uongozi wa Rais wa TFF, Wallace Karia, matumizi ya FVS yanaongeza chachu katika maboresho ya uendeshaji wa soka nchini, Ikiwa mfumo utaendelea kutumika kwa usahihi na waamuzi pamoja na makocha wakaelewa taratibu zake, unaweza kuongeza ufanisi katika maamuzi ya mchezo na kufanya Kila timu kupata haki yake bila dhuruma.

0767915473.

lugembetimothy01@gmail.com.




0/Post a Comment/Comments