ZIDANE RASMI KUINGOZA TIMU YA TAIFA YA UFARANSA

Timothy Lugembe,

Mwanakwetusports.

Zinedine Zidane ameteuliwa kuwa kocha mkuu wa timu ya taifa ya Ufaransa, hatua inayomaliza kipindi cha Didier Deschamps aliyeiongoza timu hiyo kwa zaidi ya muongo mmoja.

Uteuzi huo unamrejesha Zidane kwenye benchi la ufundi baada ya kuwa nje ya ukocha kwa takribani miaka mitano, Shirikisho la Soka la Ufaransa limempa mkataba utakaodumu hadi baada ya Kombe la Dunia la mwaka 2030.

Zidane anaanza jukumu hilo akiwa na uzoefu wa kuinoa klabu ya Real Madrid katika vipindi viwili tofauti, ambapo alifanya kazi kuanzia mwaka 2016 hadi 2018 kabla ya kurejea tena kati ya mwaka 2019 na 2021.

Akizungumza baada ya kuthibitishwa, Zidane amesema kupewa nafasi ya kuiongoza timu ya taifa ni jukumu ambalo amekuwa akiliheshimu kwa muda mrefu akisisitiza kuwa atafanya kazi kwa ushirikiano na viongozi wa shirikisho ili kutimiza malengo ya timu.

Kocha huyo pia alimshukuru rais wa Shirikisho la Soka la Ufaransa Philippe Diallo pamoja na wajumbe wa kamati ya utendaji kwa kumuamini, huku akitoa pongezi kwa Deschamps na benchi lake la ufundi kwa mchango walioutoa katika kipindi chote walichokinoa kikosi hicho.

Kwa uteuzi huo, Ufaransa inaanza kipindi kipya chini ya Zidane ambaye sasa ataanza maandalizi ya mashindano yajayo akiwa na lengo la kuijenga timu kwa miaka ijayo.

0767915473,

lugembetimothy01@gmail.com





0/Post a Comment/Comments