Timothy Lugembe,
Mwanakwetusports.
Vilabu vya Ligi Kuu Tanzania Bara NBC, NBC Championship , First league, ligi kuu ya vijana, na ligi kuu ya wanawake vitaingia kwenye msimu wa 2026/27 vikiwa na jukumu la kufanya maamuzi ya haraka sokoni baada ya dirisha kubwa la usajili kupunguzwa hadi wiki tano.
Kwa mujibu wa ratiba ya usajili ya msimu wa 2026/27, dirisha kubwa limefunguliwa Julai 6, 2026 na litafungwa Agosti 15, 2026 saa 5:59 usiku. Tofauti na misimu mingi iliyopita ambapo dirisha hilo lilikuwa likidumu kati ya wiki nane hadi 12, safari hii muda wake umepunguzwa na kuwa mfupi kuliko ilivyozoeleka.
Hiyo ina maana kuwa vilabu vitapaswa kupanga mapema mahitaji yao ya kikosi, kukamilisha mazungumzo ya usajili kwa wakati na kuepuka kuchelewa kufanya maamuzi. Katika misimu iliyopita, muda mrefu wa dirisha ulikipa kila klabu nafasi ya kuwafuatilia wachezaji kwa kina, kupima mahitaji ya timu na kisha kukamilisha usajili wake kwa sasa hali imebadilika.
Mabadiliko hayo yanakuja wakati ambapo dirisha kubwa kwa kawaida limekuwa likitumika kwa muda mrefu zaidi kuliko dirisha dogo. Kwa mujibu wa utaratibu wa kawaida wa FIFA, dirisha dogo la usajili huwa la wiki nne, huku dirisha kubwa likiwa na muda mrefu zaidi. Hata hivyo, kwa msimu huu, tofauti hiyo imepungua baada ya dirisha kubwa kubanwa hadi wiki tano.
Kupunguzwa kwa muda wa usajili kunatajwa kuchangiwa na kuchelewa kumalizika kwa mashindano ya ndani, hali iliyosababishwa na ratiba kuwa na msongamano kufuatia uwepo wa michuano ya CHAN na Matokeo yake kalenda ya maandalizi ya msimu mpya imeathirika na muda wa usajili ukalazimika kupunguzwa.
Katika mazingira hayo, vilabu vitakavyofanikiwa ni vile vitakavyoingia sokoni vikiwa tayari, vimekamilisha tathmini ya mahitaji yao na vina orodha ya wachezaji wanaowahitaji kabla ya dirisha kufungwa. Kwa msimu huu, kasi ya maamuzi inaweza kuwa sehemu ya mafanikio ya usajili.
0767915473,
lugembetimothy01@gmail.com.

Post a Comment