TIMU ZA AFRIKA NI BORA, LAKINI SI STAHILIVU

 


Timothy Lugembe,

Mwanakwetusports.

Safari ya timu za Afrika katika Kombe la Dunia 2026 imeacha picha mbili kwa wakati mmoja, Upande mmoja bara hilo limeonyesha ushindani mkubwa kwa kupeleka timu 10 kwenye mashindano Upande mwingine, limeendelea kuonyesha udhaifu wa kulinda matokeo katika michezo ya mtoano.

Mpaka sasa mashindano yamefikia hatua ya 16 Bora, huku Morocco ikiwa tayari imekata tiketi ya robo fainali na Misri ikiwa bado ipo kwenye hatua ya 16 Bora. Hiyo ina maana kuwa kati ya timu 10 za Afrika zilizoanza safari ya mashindano haya, ni mbili pekee ambazo bado zipo hai kwenye mbio za ubingwa.


Kwa ujumla, timu tisa kati ya 10 zilifanikiwa kufuzu hatua ya mtoano ya timu 32. Hata hivyo, idadi hiyo haikuendana na matokeo yaliyotarajiwa kwa sababu ni timu mbili pekee zilizoweza kusonga mbele hadi 16 Bora na zaidi. Hapo ndipo mjadala mkubwa unaanzia, Afrika ina timu zenye uwezo wa kucheza, lakini nyingi bado zinaangushwa na ukosefu wa ustahimilivu katika dakika za mwisho.

Miongoni mwa timu zilizotoka licha ya kuwa na nafasi ni DR Congo, Senegal, Ivory Coast na Afrika Kusini, timu hizo kwa nyakati tofauti zilikuwa na nafasi ya kuvuka, lakini zikashindwa kushikilia walichokuwa nacho Hali iliyo wasababisha kuishia hatua ya 32 bora.


Afrika Kusini, iliondoshwa baada ya kufungwa 1-0 na Canada Katika mchezo huo ilionekana wazi kuwa nafasi ya kusonga mbele ilikuwa mikononi mwao, Walitengeneza mazingira ya kupata matokeo, lakini wakashindwa kutumia nafasi walizozipata Kisha mwisho wa mchezo ukawa mchungu zaidi waliporuhusu bao la dakika ya 90+2, bao lililomaliza safari yao.

Ivory Coast nayo ikaondoka kwa simulizi linalofanana Ilifungwa 2-1 na Norway katika mchezo ambao walionyesha uwezo wa kurudi baada ya kutanguliwa, Norway walipata bao la kwanza dakika ya 39, lakini Ivory Coast ikapambana na kusawazisha dakika ya 74. Hapo ndipo ilipotakiwa kuonyesha utulivu kuelekea mwisho wa mchezo, lakini badala yake ikaruhusu bao la pili dakika ya 86 na kuondoshwa.


Kwa DR Congo, hadithi ilianza vizuri lakini walimaliza vibaya dhidi ya England, Congo ilitangulia mapema dakika ya saba na kwa muda mrefu ilionekana kuwa inaelekea kulinda ushindi huo. Hata hivyo, ilipofika mwisho wa mchezo, presha ikabadilisha mkondo wa matokeo ambapo England ilisawazisha dakika ya 75 kabla ya kuongeza la pili dakika ya 86, na hapo safari ya Congo ikafungwa.

Senegal ndiyo ilitoa mfano mkubwa wa namna mchezo unaweza kugeuka ndani ya dakika chache dhidi ya Belgium, Senegal ilikuwa mbele kwa mabao 2-0 hadi dakika ya 85 na wakati huo kila kitu kilionekana kuwa upande wao Lakini kuanzia hapo mchezo ukabadilika Belgium ikapindua meza dakika ya 86, na 89, na kuongeza nyundo ya tatu na kuwafanya Senegal kuondoshwa wakati wakiwa wanastahili kufuzu.

Hata hivyo, si kila timu ya Afrika iliondoka kwa lawama za kushindwa kulinda matokeo kwa upande wa Cape Verde, licha ya kufungwa 3-2 na mabingwa watetezi Argentina, timu hiyo ilipambana na kuonyesha kuwa haikuingia uwanjani kukamilisha idadi bali kupambana, Vivyo hivyo kwa Algeria, ambayo ilifungwa 2-0 na Switzerland katika mchezo ambao tofauti ya ubora wa timu hizo ndio uliamua matokeo ya mchezo huo.

Kutokana na matokeo hayo, somo kwa timu nyingi za Afrika linaonekana kuwa moja. si tatizo la uwezo wa kucheza pekee, bali ni uwezo wa kuhimili presha ya dakika za mwisho, kulinda matokeo na kuheshimu hali ya mchezo, mara kadhaa timu hizo zimeonyesha mpira mzuri, lakini zikashindwa kusimama dakika za mwisho pale mechi inapohitaji utulivu, nidhamu ya ulinzi na maamuzi sahihi.

 Macho sasa yanaelekezwa kwa Morocco na Misri, timu mbili zilizobaki kuiwakilisha Afrika. Morocco tayari imefuzu robo fainali baada ya kuifunga Canada mabao 3-0, matokeo yaliyoonyesha nidhamu ya mchezo wa mtoano na uwezo wa kutumia nafasi zilizopatikana, Misri, kwa upande wake, bado ipo hatua ya 16 Bora na inatarajiwa kuvaana na Argentina katika pambano la kusaka tiketi ya robo fainali.

Kwa namna moja au nyingine, timu hizo mbili zimeonyesha kitu ambacho timu nyingine za Afrika zilikikosa katika hatua za mtoano, subira, umakini wa ulinzi na uwezo wa kuishi ndani ya matokeo ya mchezo. Hapa ndipo hoja ya msingi inapojitokeza kuwa timu za Afrika zina ubora, lakini nyingi bado hazijawa na ustahimilivu wa kutosha wa kusimamia ushindi au matokeo muhimu pale mchezo unapofika hatua ya maamuzi

Kwa hiyo, kuelekea mashindano yajayo, somo kwa Afrika ni wazi, Ili timu zake zifike mbali zaidi kwenye michuano mikubwa ya dunia, hazihitaji tu kucheza vizuri, bali pia kujifunza namna ya kulinda walichonacho, kusoma dakika za mwisho za mchezo na kubaki na nidhamu mbele ya presha ya mpinzani, hilo ndilo daraja linaloweza kuibeba Afrika kutoka kuwa bara lenye timu zenye uwezo, hadi kuwa bara lenye timu zenye ushindani na mafanikio ya makombe.

0767915473,

lugembetimothy01@gmail.com.



0/Post a Comment/Comments