TFF kukata alama Tano kwa timu itakayo Kiuka matumizi ya vyumba vya kubadilishia nguo

Timothy Lugembe,

Mwanakwetusports.

Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) limeingiza adhabu ya kukata alama tano kwenye kanuni za mashindano ili kudhibiti ukiukaji wa taratibu za matumizi ya miundombinu ya viwanja, ikiwemo vyumba rasmi vya kubadilishia nguo.

Rais wa TFF, Wallace Karia, amesema hatua hiyo imefuatia kubainika kwa baadhi ya klabu kutumia maeneo ambayo hayajatengwa rasmi kwa shughuli hizo, jambo ambalo linakwenda kinyume na kanuni za uendeshaji wa mashindano.

Akitoa mfano, Karia amesema katika baadhi ya michezo iliyochezwa Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo, kulikuwa na matumizi ya Jumba la Maajabu badala ya vyumba rasmi vya kubadilishia nguo akieleza kuwa kuwa hali hiyo ilijitokeza katika mchezo kati ya Yanga na Simba na ikaendelea kutumika kwenye mchezo wa mwisho wa Yanga dhidi ya JKT Tanzania katika uwanja huo.

Kutokana na hali hiyo, TFF imeeleza kuwa imeanza kuboresha miundombinu kwa kununua vifaa vya kisasa kwa ajili ya vyumba vya kubadilishia nguo ili kuhakikisha timu zinatumia maeneo yaliyotengwa rasmi.

Aidha, Karia amesema vifaa hivyo vitatumika pia kuhakiki madai yanayotolewa kuhusu mazingira ya vyumba hivyo, endapo uchunguzi utaonyesha madai hayana msingi, timu husika itachukuliwa hatua kwa mujibu wa kanuni.

Kwa mujibu wa TFF, kanuni hizo zinamtaka kila mshiriki wa mashindano kufuata utaratibu wa kutumia vyumba rasmi vya kubadilishia nguo huku Klabu au timu itakayokiuka masharti hayo itakatwa alama tano kwa kila tukio la ukiukaji, kwa lengo la kuhakikisha sheria za mashindano zinafuatwa.

0767815473,

lugembetimothy01@gmail.com.



0/Post a Comment/Comments