SAMATTA ATUNDIKA DARUGA TIMU YA TAIFA

 

Timothy Lugembe,

Mwanakwetusports.

Nahodha wa Taifa Stars na mchezaji wa timu ya Le Harve ya ufaransa Mbwana Samatta, ametangaza kustaafu kuitumikia timu ya taifa ya Tanzania, akihitimisha safari ya miaka 15 ndani ya kikosi hicho akiwa na umri wa miaka 33.

Samatta ametangaza uamuzi huo kupitia ujumbe wake rasmi, akieleza kuwa baada ya kutafakari kwa kina ameona umefika wakati wa kuhitimisha jukumu lake ndani ya Taifa Stars. Mshambuliaji huyo amesema amekuwa na heshima kubwa kuvaa jezi ya Tanzania kwa kipindi chote alichokaa ndani ya timu ya taifa, huku akieleza fahari ya kuiongoza Stars kama nahodha kwa miaka 10. 

Katika kipindi chake , Samatta amekuwa sehemu ya hatua muhimu za timu hiyo. Alikiongoza kikosi kufuzu fainali za Mataifa ya Afrika mara tatu, huku pia akiwa sehemu ya timu iliyofika hatua ya 16 bora ya AFCON, hatua iliyoweka rekodi mpya kwa Tanzania katika mashindano hayo.

Mbali na uongozi wake uwanjani, Samatta ameacha alama kama mmoja wa wachezaji walioiongoza safu ya ushambuliaji ya Stars kwa muda mrefu, Katika miaka yake yote ndani ya timu ya taifa, amekuwa miongoni mwa wachezaji waliotumika kwa mechi nyingi na kutoa mchango mkubwa katika mabao na matokeo ya timu hiyo katika mashindano ya kimataifa.

Katika salamu zake za kuaga, Samatta ameishukuru Serikali, Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), familia yake, wachezaji wenzake, marafiki pamoja na mashabiki kwa ushirikiano waliompa katika kipindi chake chote akiwa na Stars ameongeza kuwa safari yake ndani ya timu ya taifa imekuwa na nyakati za furaha na huzuni, lakini ataendelea kubaki karibu na soka la Tanzania kwa namna nyingine nje ya uwanja. 

Kustaafu kwa Samatta kunafungua ukurasa mpya ndani ya Taifa Stars, huku timu hiyo ikielekea kwenye hatua ya kujenga kizazi kingine kitakachochukua majukumu aliyokuwa nayo kwa miaka mingi.

0767915473,

lugembetimothy01@gmail.com.



0/Post a Comment/Comments