RONALDO AZUA MJADALA BAADA YA KU-LIKE CHAPISHO LILILO IKOSOA FIFA

 

Timothy Lugembe,

Mwanakwetusports 

Mchezaji wa Al-Nassr na timu ya Taifa ya Ureno Cristiano Ronaldo, ameibua mjadala mtandaoni baada ya akaunti yake ya Instagram kuonyesha kuwa alipenda (ku-like) chapisho lililokuwa na kauli za mwandishi wa habari kutoka Hispania zilizokosoa FIFA na timu ya taifa ya Argentina.

Chapisho hilo lilinukuu kauli ambazo mwandishi huyo alidai kuzitoa kabla ya fainali ya Kombe la Dunia, akisema Argentina isingefika hatua hiyo bila msaada wa FIFA, Pia alidai kuwa shirikisho hilo limekuwa na ushawishi katika matokeo ya mashindano.

Katika nukuu hizo, mwandishi huyo alisema hakuwa na hofu na Argentina bali alikuwa na hofu na Rais wa FIFA, Gianni Infantino aliongeza kuwa aliamini timu yake isingekuwa ikicheza dhidi ya Argentina pekee, bali pia dhidi ya FIFA.

Aidha, mwandishi huyo alidai kuwa FIFA ilitaka Lionel Messi anyanyue Kombe la Dunia kama ilivyotokea katika mashindano ya mwaka 2022 nchini Qatar.

Mbali na madai hayo, aligusia suala la bei za tiketi akisema zimewafanya mashabiki wengi kushindwa kuhudhuria michezo, hali aliyodai imepunguza ushiriki wa mashabiki wa kawaida katika mashindano hayo.

Pia alimlaumu mwandaaji wa mashindano kwa kile alichokiita uendeshaji usiofaa wa tukio hilo, huku akieleza kuwa angeendelea kufuatilia michezo licha ya kutoridhishwa na namna mashindano yalivyoandaliwa.

Hatua ya Ronaldo ku-like chapisho hilo imeendelea kuzua mijadala kwenye mitandao ya kijamii, huku baadhi ya watumiaji wakitafsiri kitendo hicho kama kuunga mkono maoni yaliyotolewa na mwandishi huyo. Hata hivyo, Ronaldo hajatoa tamko rasmi kueleza sababu za ku-like chapisho hilo, na FIFA pia haijajibu madai yaliyomo kwenye chapisho hilo.

0767915473,

lugembetimothy01@gmail.com.



0/Post a Comment/Comments