Mshauri wa Infantino ajiuzulu kupinga mpango wa FIFA kuuza hisa za Kombe la Dunia

Timothy Lugembe,

Mwanakwetusports.

Mshauri Mkuu wa Rais wa FIFA, Carlos Cordeiro, amejiuzulu wadhifa wake baada ya kupinga mpango wa shirikisho hilo wa kuuza sehemu ya hisa kwenye shughuli za mashindano ya Kombe la Dunia kwa wawekezaji binafsi.

Cordeiro alisema hakuwa sehemu ya maandalizi ya pendekezo hilo na haungi mkono uamuzi wa FIFA kuanzisha utaratibu huo, ameeleza kuwa hawezi kuendelea kuhudumu katika nafasi hiyo wakati shirikisho linafikiria kuuza hisa za mashindano ambayo yana nafasi kubwa katika soka la dunia.

Aidha, alibainisha kuwa msimamo wake unatokana na imani yake kuhusu mustakabali wa Kombe la Dunia, akisisitiza kuwa alipinga pendekezo hilo tangu lilipoibuliwa.

Cordeiro, mwenye umri wa miaka 70, amekuwa mshauri mkuu wa Rais wa FIFA, Gianni Infantino, kwa kipindi cha miaka mitano baada ya kufanya kazi kwa muda mrefu katika sekta ya uwekezaji wa kifedha.

Wiki hii, FIFA ilitangaza mpango wa kuanzisha kampuni mpya itakayosimamia mashindano yake makubwa, ikiwemo Kombe la Dunia Kupitia kampuni hiyo, shirikisho linakusudia kuuza sehemu ndogo ya hisa kwa wawekezaji binafsi huku likieleza kuwa hatua hiyo inalenga kuimarisha usimamizi wa shughuli zake.

Hata hivyo, tangazo hilo limeibua mjadala ndani na nje ya soka, huku kujiuzulu kwa Cordeiro kukiwa ishara ya kutokubaliana na mwelekeo huo wa uongozi wa FIFA.

0767915473,

lugembetimothy01@gmail.com.



0/Post a Comment/Comments