FIFA yapanga kuongeza muda wa mapumziko fainali ya Kombe la Dunia 2026


Timothy Lugembe,

Mwanakwetusports.

Shirikisho la Mpira wa Miguu Duniani (FIFA) linatarajia kufanya mabadiliko katika fainali ya Kombe la Dunia 2026 kwa kuongeza muda wa mapumziko ya kipindi cha kwanza ili kutoa nafasi ya burudani maalum itakayofanyika wakati wa mapumziko.

 Mapumziko ambayo kwa kawaida huchukua dakika 15 yanaweza kuongezwa hadi dakika 20, huku ripoti nyingine zikieleza kuwa yanaweza kufikia dakika 30. Hatua hiyo inalenga kuwezesha burudani ya kiwango kikubwa.

Burudani hiyo inatarajiwa kufanyika katika Uwanja wa MetLife katika mchezo wa fainali utakao wakutanisha timu ya Taifa ya Hispania dhidi ya Argentina , FIFA inaelezwa kutaka kuifanya fainali hiyo kuwa tukio linalounganisha soka na burudani mbele ya mamilioni ya watazamaji duniani huku burudani ikitarajiwa kutolewa na wasanii mbali mbali wakiwemo Shakira, Madonna, Justin Bieber, BTS na Coldplay.

Mabadiliko hayo yamezua mjadala ndani ya ulimwengu wa soka, kutokana na Sheria za Mchezo kuelekeza kuwa mapumziko ya kipindi cha kwanza hayapaswi kuzidi dakika 15. Wapo wanaohoji kuwa kuongeza muda wa mapumziko kunaweza kuathiri maandalizi na hali ya kimwili ya wachezaji kabla ya kipindi cha pili kuanza.

Iwapo mpango huo utapitishwa, fainali ya Kombe la Dunia 2026 itakuwa ya kwanza katika historia ya mashindano hayo kuwa na burudani maalum ya mapumziko kwa kiwango kinachofanana na Super Bowl, hatua ambayo FIFA inaamini itaongeza mvuto wa tukio hilo kwa mashabiki wa soka na burudani duniani.

0767915473,

lugembetimothy01@gmail.com





0/Post a Comment/Comments