USAJILI ULAYA: AC Milan Yamnasa Amorim, Mustakabali wa Rashford Bado Wazi

Timothy Lugembe,

Mwanakwetusports.

Milango ya dirisha la usajili ilipofunguliwa, AC Milan ikavua ukurasa wa zamani na kuandika sura mpya kwa kumkabidhi Ruben Amorim funguo za kikosi chake, Wakati Rossoneri wakitazama mbele kwa matumaini mapya, macho ya Ulaya yameelekezwa Manchester United ambako mustakabali wa Marcus Rashford unaendelea kuwa moja ya simulizi kubwa  za usajili msimu huu.

AC Milan imemtangaza rasmi Amorim kuwa kocha mkuu mpya wa klabu hiyo kwa mkataba wa miaka miwili utakaomalizika Juni 2028, ukiwa na chaguo la kuongeza mwaka mmoja zaidi, Uteuzi huo unakuja baada ya klabu hiyo kufanya tathmini ya msimu uliopita ambapo ilishindwa kufikia malengo yake na kumaliza katika nafasi ya tano kwenye Serie A.

Kocha huyo mwenye umri wa miaka 41 anawasili San Siro akiwa na sifa ya kuwa mmoja wa makocha vijana walioonyesha mafanikio makubwa katika soka la Ulaya. Akiwa Sporting CP, Braga, Casa pia, na Manchester United.

Uongozi wa Milan unaamini ujio wake utaleta mabadiliko ya kiufundi na kimfumo, hasa wakati klabu hiyo ikijiandaa kwa msimu mpya wenye ushindani ndani ya Italia na katika mashindano ya Ulaya.

Wakati Milan ikifanya mabadiliko kwenye benchi la ufundi, Manchester United imejikuta katika presha ya kumaliza mjadala kuhusu mustakabali wa Marcus Rashford, Mshambuliaji huyo wa kimataifa wa England ameendelea kuhusishwa na klabu mbalimbali za Ulaya huku ripoti zikidai kuwa ana kipengele cha kuondoka kwa ada ya pauni milioni 40.

Barcelona imeendelea kutajwa kuwa miongoni mwa klabu zinazovutiwa na huduma za Rashford. Mabingwa hao wa Hispania wanatafuta njia ya kuimarisha safu yao ya ushambuliaji na wanaamini uzoefu wa nyota huyo unaweza kuongeza ushindani katika kikosi chao, hata hivyo, taarifa zinaonyesha kuwa klabu hiyo inapendelea kwanza mpango wa mkopo kabla ya kufikiria usajili wa moja kwa moja.

Kadri dirisha la usajili linavyoendelea, suala la Rashford linaweza kuwa moja ya habari zitakazotawala vichwa vya habari vya soka barani Ulaya, Wakati AC Milan ikianza safari mpya chini ya Amorim, Manchester United nayo inasubiri kuona kama itaendelea kuwa na mmoja wa nyota wake au atapewa mkono wa kwa heri.

Kwa sasa, mashabiki wa soka duniani wanaendelea kufuatilia kwa karibu kila hatua inayofanyika katika soko la usajili, huku Amorim na Rashford wakiwa miongoni mwa majina yanayovuta hisia zaidi katika kipindi hiki cha maandalizi ya msimu mpya.

0757915473,

lugembetimothy01@gmail.com.

0/Post a Comment/Comments