Timothy Lugembe,
Mwanakwetusports.
Timu ya Taifa ya Uholanzi imeendelea kuandika rekodi ya kutopoteza mchezo wowote ndani ya dakika 90 za Kombe la Dunia tangu mwaka 2006 walipo fungwa na ureno bao 1-0 katika Fainali zilizofanyiaka nchini ujerumani wakiondoshwa katika hatua ya 16 Bora.
Historia hiyo inaendelea kuishi baada ya miamba hiyo kumaliza hatua ya makundi ya michuano ya mwaka 2026 ikiwa na ushindi katika michezo miwili na sare moja, Matokeo hayo yameifanya iingie hatua ya mtoano ikiwa bado haijapoteza ndani ya muda wa kawaida wa mchezo.
Rekodi hiyo imeendelea kudumu kwa takribani miaka 20, licha ya Uholanzi kushindwa kutwaa taji la Kombe la Dunia katika mashindano yaliyopita kutokana na kuondolewa katika hatua za mtoano kupitia dakika za nyongeza au mikwaju ya penalti.
Baada ya kufungwa mara ya mwisho 2006, Miaka minne baadaye, Uholanzi ilifika fainali ya Kombe la Dunia 2010 nchini Afrika Kusini, lakini ikapoteza mchezo kwa bao 1-0 dhidi ya Hispania baada ya Andres Iniesta kufunga bao la ushindi katika dakika ya 116 ya muda wa nyongeza.
Katika Kombe la Dunia la mwaka 2014 nchini Brazil, Uholanzi ilifika hatua ya nusu fainali kabla ya kuondolewa na Argentina kwa mikwaju ya penalti 4-2, kufuatia mchezo uliomalizika kwa sare ya bila kufungana ndani ya dakika 120.
Uholanzi haikufuzu kushiriki Kombe la Dunia la mwaka 2018 nchini Urusi, kabla ya kurejea katika fainali za mwaka 2022 nchini Qatar , hata hivyo, safari yake iliishia robo fainali baada ya kuondolewa na Argentina kwa mikwaju ya penalti 4-3 kufuatia sare ya mabao 2-2 ndani ya dakika 120.
Sasa, katika Kombe la Dunia la mwaka 2026, Uholanzi imeanza tena safari ya kusaka taji kwa kuonyesha mwenendo mzuri katika hatua ya makundi. Ikiwa haijapoteza mchezo wowote ndani ya dakika 90 na tayari imefuzu hatua ya mtoano, timu hiyo inaendelea kubeba rekodi yake ya kipekee huku ikionekana kuwa miongoni mwa timu zenye nafasi ya kufanya vizuri katika mbio za ubingwa.
0767915473,
lugembetimothy01@gmail.com.



Post a Comment