Adeladius Makwega – Musoma, MARA, TANZANIA.
Timu ya soka ya Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa MARA, maarufu kama RAS MARA, imetwaa ubingwa wa miaka 30 ya TRA Mkoa wa Mara baada ya kuichabanga bila majibu wala huruma timu ya Manispaa ya Musoma kwa magoli matatu kwa bila.
Mechi hiyo ya fainali, iliyochezwa Juni 27, 2026 wilayani Musoma, ilianza kwa gonga na pasi fupi fupi, ambapo hadi kipindi cha kwanza kinamalizika ubao wa magoli ulikuwa wa bila bila. Baada ya mapumziko, dakika saba baadaye, vijana wa Ras Mara waliibuka na kutia kimiani bao lao la kwanza, lililotumbikizwa kimiani na mchezaji wao mahiri Omari Omari. Nyota ya Ras Mara ilizidi kung’aa na, baada ya dakika tatu tu, mchezaji wao mahiri Samson David alifunga bao la pili na kufanya wachezaji wa Manispaa ya Musoma kuchanganyikiwa na kupata bumbuwazi, mithili ya mtu asiyejua kuongelea aliyetupwa katikati ya Ziwa Victoria.
Mashambulizi yalikuwa makali sana na, dakika mbili kabla ya kipenga cha mwisho, Omari Omari kwa mara ya pili alitumbikiza kimiani bao la tatu la Ras Mara na mpira kuwekwa dimbani. Harakaharaka, hapo hapo, mipira mirefu mirefu ilipigwa kwa dakika moja unusu, Manispaa ya Musoma wakihaha hoi bin taabani , ulimi nje,walikoswa koswa kufungwa bao la nne, ambalo Ras Mara walitafuta kwa uvumba na ubani ili kila mchezaji wa Manispaa ya Musoma wagawane robo robo ya maumivu hayo ya kufungwa, lakini kipenga cha muamuzi kiliwaonea huruma Manispaa ya Musoma na mchezo kuhitimishwa kwa Ras Mara kushinda magoli matatu, na Manispaa ya Musoma haikupata kitu.
Aidha, katika mchezo wa netiboli, Manispaa ya Musoma ilikuwa bingwa, Ras Mara Malkia kutoka Mlima Mukendo wakishika nafasi ya pili.
Michezo hiyo pia iliambatana na kukimbiza na kukamata kuku, ambapo mchezaji wa Ras Mara, Gideon Chilongani, chupuchupu amkamate kuku lakini alipiga dafrao moja matata na kuanguka chini. Huku jamaa wa huduma ya kwanza walimkimbilia na kumbeba kumpa huduma ya kwanza nje ya uwanja, kuku huyu alimpiga chenga ya mwili na kumtoroka, ambapo mshindi wa kukamata kuku alipatikana baada ya kurudiwa mara tatu.
Katika mashindano ya riadha ya mita 100, mchezaji mahiri wa Ras Mara, Gladness Shayo, alishika nafasi ya tatu, ambapo alikimbia nje ya kiwango chake kutokana na mazingira ya kiwanja hayakuwa mazuri na vumbi lilikuwa kali.
Akijinasibu kandoni mwa mashindano hayo, kiongozi wa timu ya Ras Mara, Hashimu Ujonjo, amesema kuwa huo ni mwanzo mzuri na kwa hakika mafanikio ya vikosi vyao vyote kwa michezo yote ni asilimia 77, huku kwa asilimia 65 wamechezesha vikosi namba mbili, ambapo vikosi namba moja vipo kambini kwa ajili ya mashindano mengine ya kitaifa.
“Kwa sasa tunachezesha vikosi vya pili ili kuchuja na kupata wachezaji bora zaidi katika vikosi vya kwanza, iwe katika soka, netiboli, riadha, kukimbia na magunia, kukimbiza kuku, kuvuta kamba na michezo mingine.”
Akizungumza katika hafla hiyo ya miaka 30 ya TRA, Mkuu wa Wilaya ya Musoma, Mheshimiwa Juma Chikoka, aliwapongeza Ras Mara kufanya vizuri katika mashindano hayo huku akiomba timu zingine ziongeze nguvu katika michezo hiyo. Mkuu wa Wilaya ya Musoma pia alisisitiza suala la amani kwa kila mwana Musoma.
“Bila amani hatuwezi kufanya lolote lile la maendeleo. Naombeni tuwe watulivu ili kila mmoja atekeleze majukumu yake ili mwisho kila mmoja ajipatie ridhiki.”
Kwa upande wake, Meneja wa TRA Mkoa wa Mara, ndugu Masawa Masatu, alitumia fursa hiyo kujitambulisha kwa wana Mara, akisema yeye ni mgeni, anapiga hodi mkoani Mara na anaomba apokelewe.
“Nawaombeni sana mlipe kodi ambazo ndizo zinazotumika kulipia miradi kadhaa ya maendeleo.”
Wakati haya yakiendelea hapa Musoma, hali ya hewa ya mji wa Musoma ni nyuzi joto 28, uwezekano wa mvua ni asilimia 46, upepo ukivuma kwa KM 19 kwa saa.
makwadeladius@gmail.com
0717649257
.gif)











.gif)
Post a Comment