ONANA AREJEA UNITED, TRABZONSPOR WANAMUHITAJI TENA

 

Timothy Lugembe,

Mwanakwetusports.

Kipa wa kimataifa wa Cameroon, Andre Onana, amerejea katika kikosi cha Manchester United kwa ajili ya maandalizi ya msimu mpya chini ya kocha Michael Carrick baada ya kumaliza kipindi chake cha mkopo katika klabu ya Trabzonspor ya nchini Uturuki.

Taarifa kutoka vyombo mbalimbali vya michezo Ulaya zinaeleza kuwa Onana anatarajiwa kujiunga na kambi ya maandalizi ya United huku hatma yake ikiwa bado haijafahamika rasmi, licha ya klabu hiyo kuonekana kuwa tayari kuachana naye dirisha hili la usajili.

Inaelezwa kuwa Trabzonspor bado ina nia ya kuendelea kubaki na kipa huyo kwa mkopo mwingine kutokana na kiwango kizuri alichokionesha, ambapo alisaidia timu hiyo kumaluza nafasi ya tatu kwenye ligi hiyo.


Hata hivyo, changamoto kubwa inayoweza kuzuia dili hilo ni mshahara mkubwa wa Onana ndani ya Manchester United, jambo linalodaiwa kuwapa wakati mgumu Trabzonspor pamoja na vilabu vingine vinavyomuhitaji.

Kwa upande mwingine, baadhi ya ripoti zinaeleza kuwa Onana mwenyewe bado anaamini ana nafasi ya kurejea na kupigania namba ndani ya United, licha ya ujio wa kipa mpya Senne Lammens ambaye ameonekana kuaminiwa zaidi Old Trafford.

Mazungumzo kati ya pande husika yanatarajiwa kuendelea wiki hizi za dirisha la usajili huku mustakabali wa kipa huyo ukiendelea kuzua mjadala mkubwa miongoni mwa mashabiki wa soka Ulimwenguni.

0767815473,

lugembetimothy01@gmail.com.


0/Post a Comment/Comments