Timothy Lugembe,
Mwanakwetusports.
Sare ya mabao 1-1 dhidi ya Brazil imeendelea kuonyesha kuwa Morocco si miongoni mwa timu zinazoshiriki Kombe la Dunia kwa ajili ya kuongeza idadi, bali ni moja ya mataifa ya Afrika yanayoweza kutoa changamoto kwa vigogo wa soka duniani.
Tofauti na Kombe la Dunia la 2022 ambapo walitegemea zaidi mashambulizi ya kushtukiza (counter attack) na uimara wa safu ya ulinzi, Morocco ya sasa inaonyesha sura mpya, timu hiyo inamiliki mpira kwa muda mrefu, inajenga mashambulizi kwa utulivu na kucheza kwa kasi kubwa bila kuogopa kukabiliana na mataifa makubwa. Mtindo huo uliwawezesha kusimama imara dhidi ya Brazil na kuonyesha kuwa wana uwezo wa kushindana kwa kiwango cha juu.
Miongoni mwa waliovutia ni kiungo wa miaka 18 wa klabu ya Lille OSC, Ayyoub Bouaddi, ambaye alionyesha kiwango kikubwa katika mchezo huo.
Bouaddi alikamilisha pasi 60 kati ya 66 kwa usahihi wa asilimia 91, akafikisha pasi zote 16 alizocheza katika eneo la mwisho la ushambuliaji, akarejesha mipira sita, akafanya interceptions tano na kushinda mapambano tisa ya ana kwa ana, Takwimu hizo zimeendelea kumuweka miongoni mwa vipaji vinavyofuatiliwa kwa karibu katika soka la dunia.
Morocco sasa itaelekeza nguvu zake katika mchezo unaofuata dhidi ya Scotland utakaochezwa Juni 20, kabla ya kuhitimisha hatua ya makundi dhidi ya Haiti Juni 25.
Kwa kiwango kinachoonyeshwa sasa, Morocco imejijengea hadhi ya kuwa moja ya timu tishio kutoka Afrika katika Kombe la Dunia, iwapo itaendelea na mwenendo huu, inaweza kufikia au hata kuvuka rekodi yake ya mwaka 2022 ilipofika hatua ya nusu fainali na kuweka historia kwa bara la Afrika.
0767915473,
lugembetimothy01@gmail.com.



Post a Comment