Timothy Lugembe
Mwanakwetusports.
Hali ya sintofahamu imeibuka baada ya mwamuzi bora wa Afrika mwaka 2025, Omar Abdulkadir Artan, kuzuiwa kuingia nchini Marekani alipowasili kwa ajili ya maandalizi ya michuano ya Kombe la Dunia 2026.
Mwamuzi huyo kutoka Somalia alitarajiwa kuwa raia wa kwanza wa taifa hilo kuchezesha Kombe la Dunia, hatua ambayo ingeandika historia kubwa katika soka la nchi hiyo pamoja na yeye binafsi.
Kwa mujibu wa taarifa zinazosambaa, Artan alizuiwa kuingia Marekani kabla ya kurejeshwa nchini Uturuki, huku sababu rasmi za uamuzi huo zikiwa bado hazijawekwa wazi hadi sasa.
Baada ya zuio hilo, shirikisho la mpira wa miguu Duniani FIFA limethibitisha kuwa mwamuzi huyo hatakuwa sehemu ya mashindano hayo baada ya kuzuiwa kuingia nchini Marekani kwaajili ya maandalizi ambapo nchi hiyo ni moja ya waandaji wa mashindano hayo.
Ikumbukwe kuwa nchi ya Somalia ni miongoni mwa nchi zilipopigwa marufuku yakusafiri kuelekea Marekani chini ya uongozi wa Rais Donald Trump, huenda ikawa sababu kwa makisio lakini sababu rasmu hazijatolewa.
Artan alikuwa amepewa nafasi kubwa ya kuwa sehemu ya waamuzi watakaochezesha Kombe la Dunia 2026, jambo ambalo lingeiweka Somalia kwenye ramani ya soka la dunia kupitia sekta ya waamuzi.
Hivyo safari ya kuandika historia mpya katika tasnia yake na ndoto ya kuchezesha mashindano makubwa ngazi ya Dunia rasmi imefia uwanja wa ndege wa Miami nchini Marekani.
Wakati taarifa zaidi zikisubiriwa, tukio hilo limeendelea kuzua mjadala mkubwa katika mitandao ya kijamii na miongoni mwa mashabiki wa soka barani Afrika.
0767915473,
lugembetimothy01@gmail.com.



Post a Comment