LA MASIA YAMPOKEA KINDA WA TANZANIA , MATUMAINI YAONGEZEKA KWA SOKA LA VIJANA

 

Timothy Lugembe,

Mwanakwetusports.

Soka la vijana nchini Tanzania linaendelea kupiga hatua huku vijana wengi wakianza kupata nafasi ya kujiunga na akademi na klabu kubwa nje ya nchi, mafanikio hayo yanaonyesha kuwa vipaji vya vijana wa Kitanzania vinaanza kuonekana kimataifa kupitia mashindano ya vijana na akademi mbalimbali zinazowakuza wachezaji wenye uwezo.

Hivi karibuni, kinda raia wa Tanzania, Barka Seif, amejiunga na akademi ya FC Barcelona maarufu kama LA MASIA iliyopo nchini Hispania, akademi hiyo ni moja ya vituo vikubwa vya kuzalisha vipaji duniani baada ya kutoa mastaa wengi waliotikisa soka la dunia.

Baadhi ya nyota waliopitia LA MASIA ni pamoja na Lionel Messi, Xavi Hernandez, Andres Iniesta pamoja na nyota wa sasa Lamine Yamal ambaye ameendelea kuonyesha kiwango kikubwa akiwa na Barcelona pamoja na timu ya taifa ya Hispania akiwa na umri mdogo.

Barka amejiunga na LA MASIA akitokea Damm Football Academy, hatua inayotazamwa kama mafanikio kwa maendeleo ya soka la vijana Tanzania. Kujiunga kwake kwenye mfumo wa maendeleo wa Barcelona kunafungua nafasi kwa vijana wengine kuamini kuwa wanaweza kufikia viwango vikubwa kupitia mafunzo na ushindani wa kimataifa.

Kabla ya taarifa hiyo, kiungo wa Serengeti Boys, Issa Musa Chole, aliwahi kuhusishwa na klabu mbalimbali za Ulaya ikiwemo Slavia Prague baada ya kuonyesha kiwango kizuri katika mashindano ya vijana U-17 yaliyofanyika nchini Morocco 2026. Hali hiyo iliongeza matumaini kwa mashabiki wa soka kuhusu uwezo wa vijana wa Tanzania kupata nafasi katika soka la kimataifa.

Kuongezeka kwa vijana wanaovutiwa na timu na akademi za nje kunatajwa kuwa matokeo ya uwekezaji wa akademi za ndani pamoja na mashindano ya vijana ambayo yanaendelea kutoa jukwaa la kuonyesha vipaji.

0767915473,

lugembetimothy01@gmail.com.


0/Post a Comment/Comments