Timothy Lugembe,
Mwanakwetusports.
Kocha mpya anapoingia ndani ya timu, mashabiki wengi hutegemea kuona mabadiliko ya haraka ndani ya uwanja, wengine hutaka kuona mfumo mpya wa uchezaji, ushindi na matokeo ndani ya michezo michache ya mwanzo, Lakini katika soka la kisasa, kazi ya kwanza ya kocha huwa si kufundisha mbinu pekee, bali kujenga uelewa wa tabia za wachezaji wake.
Ndani ya miezi ya miwili mpaka mitatu ya mwanzo, makocha wengi hutumia muda mwingi kufanya tathmini ya kikosi, Kipindi hicho hutumika kujua aina ya wachezaji waliopo, namna wanavyoitikia maelekezo, uwezo wao wa kubadilika pamoja na mwenendo wao ndani na nje ya uwanja.
Katika hatua hiyo, kocha hukutana na aina tofauti ya tabia za wachezaji. Wapo wenye hasira za haraka, wenye kiburi kutokana na majina au uwezo wao, wenye dharau kwa wenzao au maelekezo ya benchi la ufundi, pamoja na wale wenye tabia ya kujiskia kuwa wao ni muhimu zaidi ndani ya timu, tabia hizi zinaweza kuathiri nidhamu, ushindani wa nafasi na mshikamano wa kikosi ikiwa hazitadhibitiwa mapema.
Mbali na tabia hizo, kocha pia huanza kupima uwezo wa kila mchezaji kuelewa mfumo mpya wa uchezaji. Katika soka, si kila mchezaji hujifunza kwa haraka, Wapo wanaoelewa maelekezo mapema, wengine huchukua muda wa wastani huku wengine wakihitaji muda mrefu kabla ya kuendana na mfumo wa timu.
Kutokana na hali hiyo, baadhi ya makocha hutumia mgawanyo wa aina tatu za wachezaji; “golden players”, “silver players” na “iron players”.
“Golden players” huwa ni wale wanaoelewa haraka mbinu mpya, wanaotekeleza maelekezo kwa usahihi na wanaobadilika kirahisi kulingana na mfumo wa kocha, Mara nyingi hawa ndio huwa msingi wa kikosi cha kwanza.
“Silver players” ni wale wanaohitaji muda wa kati kuelewa mfumo mpya, hawa huendelea kukua taratibu kupitia mazoezi na ushindani wa ndani ya timu.
Kwa upande wa “iron players”, hawa huhitaji muda mkubwa zaidi kubadilika na kuelewa, Mara nyingi kocha hulazimika kutumia muda wa ziada kuwajenga kimfumo na kisaikolojia ili waweze kuendana na kasi ya timu.
Baada ya tathmini zote hizo ndipo kocha huanza kuunda makundi ya ndani kwa ajili ya mafunzo, nidhamu na ushindani wa nafasi. Hatua hiyo hufanyika taratibu bila wachezaji kutambua moja kwa moja.
Ndani ya kipindi hicho ndipo kikosi cha kwanza huanza kuonekana, mara nyingi si suala la majina makubwa pekee, bali ni mchanganyiko wa nidhamu, uelewa wa mfumo, uwezo wa kutekeleza majukumu na tabia ya mchezaji ndani ya timu.
Ndiyo maana wakati mwingine kocha mpya anaweza kuchelewa kupata matokeo makubwa ndani ya muda mfupi Kabla ya mbinu kufanya kazi uwanjani, kocha huhitaji kwanza kuelewa akili, tabia na mwenendo wa wachezaji wake.
0767915473,
lugembetimothy01@gmail.com.


Post a Comment