Timothy Lugembe,
Mwanakwetusports.
Ni kukosa bahati au kutojua namna ya kucheza fainali? Hilo ndilo swali ambalo limeendelea kujitokeza baada ya Tanzania kupoteza fainali tatu za mashindano ya Afrika ndani ya vipindi tofauti wakati ambao timu zikiwa kwenye kiwango bora.
Kwa mara ya kwanza msimu wa 2022/23, klabu ya Yanga ilifika fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika na kukutana na USM Alger ya Algeria.
Katika mchezo wa kwanza uliochezwa Uwanja wa Benjamin Mkapa, Yanga ilipoteza kwa bao 2-1 kabla ya kushinda bao 1-0 nchini Algeria kwenye mchezo wa marudiano. Hata hivyo, sare ya jumla ya mabao 2-2 iliifanya Yanga kukosa ubingwa kwa kanuni ya bao la ugenini.
Baada ya hapo, msimu wa 2024/25, Simba SC ilifika fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika ikiwa kwenye ushindani mkubwa ikikutana na RS Berkane ya Morocco katika michezo miwili ya fainali.
Mchezo wa kwanza nchini Morocco ulimalizika kwa Berkane kushinda mabao 2-0, huku Katika mchezo wa marudiano uliochezwa Uwanja wa New Amaan Complex Zanzibar, Simba ilitoa sare ya bao 1-1 matokeo yaliyoifanya Berkane kutwaa ubingwa kwa jumla ya mabao 3-1.
Mwaka 2026, timu ya taifa ya vijana chini ya umri wa miaka 17, Serengeti Boys, nayo iliingia fainali ya Afrika kwa mara ya kwanza dhidi ya vijana wa Senegal, baada ya kufanya vizuri katika hatua za awali za mashindano.
Katika mchezo huo wa fainali, Serengeti Boys ilitoka sare ya bao 1-1 ndani ya dakika 90 kabla ya kupoteza kwa mikwaju ya penalti 4-3 na kuikosa nafasi ya kutwaa taji.
Matokeo hayo yanaifanya Tanzania kuendelea kusubiri ubingwa wa Afrika licha ya timu zake kufanikiwa kufika hatua za mwisho za mashindano hayo.
Hata hivyo, maendeleo ya timu za Tanzania katika mashindano ya Afrika yanaonyesha mabadiliko ya ushindani ukilinganisha na miaka iliyopita, Ushiriki wa timu katika hatua za mwisho umeendelea kuongeza uzoefu kwa wachezaji na benchi la ufundi.
Kwa upande mwingine, uwekezaji katika soka pamoja na maendeleo ya vijana unaendelea kutoa matumaini ya Tanzania kufanya vizuri zaidi katika mashindano yajayo ya Afrika na dunia huku macho na masikio yakielekezwa nchini Quatar kwenye kombe la Dunia la vijana Kuona kama vijana hao watafanikiwa kuandika historia mpya katika soka la Tanzania.
0767915473,
lugembetimothy01@gmail.com.


Post a Comment