Timothy Lugembe,
Mwanakwetusports.
Shirikisho la Soka nchini Mali (FEMAFOOT) limeripotiwa kuchukizwa na uamuzi wa kocha raia wa DR Congo, anaeinoa klabu ya Azam fc , Florent Ibenge, baada ya kujiondoa kwenye mchuano wa kugombea nafasi kuinoa timu ya taifa ya nchi hiyo akieleza kuwa ana changamoto za kifamilia.
Taarifa kutoka ndani ya viongozi wa soka Mali zinaeleza kuwa Ibenge alikuwa tayari amepitia hatua mbalimbali za usaili na kuonekana kama mgombea aliyekuwa akipewa nafasi kubwa ya kuchukua mikoba ya kuifundisha timu hiyo ya taifa.
Inaelezwa kuwa majadiliano kati ya pande hizo yalikuwa yamefikia hatua nzuri kabla ya kocha huyo kuwataarifu viongozi wa FEMAFOOT kuwa hataweza kuendelea na kazi hiyo kutokana na sababu binafsi za kifamilia.
Baadhi ya viongozi ndani ya shirikisho hilo wanaamini muda mwingi ulipotea wakisubiri majibu ya Ibenge huku wakidai kama sababu hizo zilikuwepo tangu mwanzo, basi angeziweka wazi mapema ili wapate nafasi ya kuangalia makocha wengine.
Hatua hiyo sasa imewaacha viongozi wa soka Mali wakianza upya mchakato wa kutafuta kocha mpya atakayeiongoza timu ya taifa kuelekea mashindano yajayo ya kimataifa.
Kwa upande wa Ibenge, bado hajatoa maelezo ya kina kuhusu changamoto hizo za kifamilia zilizomfanya ashindwe kuichukua kazi hiyo iliyokuwa ikisubiriwa kwa hamu kubwa nchini Mali.
0767915473,
lugembetimothy01@gmail.com.


Post a Comment