Timothy Lugembe,
Mwanakwetusports.
Ujerumani imeanza kampeni ya Kombe la Dunia 2026 kwa ushindi wa mabao 7-1 dhidi ya Curaçao katika mchezo wa Kundi E, matokeo ambayo yameandika historia mbili tofauti ndani ya michuano hiyo.
Kwanza, mchezo huo umekuwa wa kwanza katika mzunguko wa ufunguzi wa Kombe la Dunia 2026 kushuhudia mabao mengi zaidi, ambapo jumla ya mabao manane yalifungwa ndani ya dakika 90.
Ushindi huo pia umeibua kumbukumbu za Kombe la Dunia 2014, ambapo Ujerumani iliifunga Brazil mabao 7-1 katika hatua ya nusu fainali kabla ya kutwaa ubingwa kwa kuifunga Argentina bao 1-0 kwenye fainali.
Mbali na idadi kubwa ya mabao, mchezo huo umeandika historia nyingine kwa kuwa wa kwanza katika mzunguko wa kwanza kumalizika bila mwamuzi kutoa kadi yoyote kwa wachezaji wa pande zote mbili, jambo lililoonyesha kiwango cha nidhamu kilichokuwepo uwanjani.
Kwa upande wa Curaçao, taifa hilo ni miongoni mwa nchi zenye idadi ndogo ya watu katika Kombe la Dunia la mwaka huu, likiwa na takribani wakazi 158,000 na eneo la kilomita za mraba 444.
Pamoja na ukubwa wa matokeo hayo, tofauti ya uwezo, uzoefu na rasilimali za soka kati ya timu hizo mbili ilifanya wengi kutarajia ushindani mgumu kwa Curaçao dhidi ya moja ya mataifa yenye historia kubwa katika michuano hiyo.
Matokeo hayo yanaifanya Ujerumani kuanza vyema safari yake ya kutafuta taji la pili la Kombe la Dunia ndani ya kipindi cha miaka 12 tangu ilipotwaa ubingwa mwaka 2014.
0767915473.
lugembetimothy01@gmail.com




Post a Comment