Timothy Lugembe,
Mwanakwetusports.
Cape Verde imeandika historia kwa kufuzu hatua ya 32 bora ya Kombe la Dunia 2026 katika ushiriki wake wa kwanza kwenye mashindano hayo, baada ya kumaliza katika nafasi ya pili ya Kundi H ikiwa na alama tatu.
Taifa hilo lilifika hatua hiyo baada ya kutoka sare katika michezo yake mitatu ya kundi, huku ikifunga mabao mawili na kufungwa mawili, Matokeo hayo yamewawezesha kumaliza nafasi ya pili nyuma ya vinara Spain.
Katika safari hiyo ya mafanikio huwezi acha kulitaja jina la golikipa wa timu hiyo Vozinha ambaye ameibuka shujaa tangu mchezo wa kwanza dhidi ya Spain kwa kutoruhusu bao na kuisaidia timu yake kuondoka na alama mbele ya miamba namba mbili ya soka Duniani, kipa huyo katika michezo mitatu karuhusu bao mbili pekee na kuchangia kwa kiasi kikubwa timu yake kusonga mbele.
Ikumbukwe kuwa Kabla ya kuanza kwa mashindano, Cape Verde ilikuwa miongoni mwa timu za Afrika zilizopewa nafasi ndogo ya kusonga mbele, Hata hivyo, imefanikiwa kufuzu moja kwa moja kutoka hatua ya makundi bila kutegemea nafasi za timu bora zilizomaliza katika nafasi za tatu(best looser).
Kufuzu huko pia kumekuwa sehemu ya historia ya soka la nchi hiyo, Mbali na kushiriki Kombe la Dunia kwa mara ya kwanza, Cape Verde imefanikiwa kufunga mabao mawili, kupata alama tatu na sasa imefuzu kwa mara ya kwanza hatua ya mtoano tofauti na mataifa mengi madogo ambayo yalishawahi kupata nafasi hiyo kwa mara ya kwanza.
Kwa upande wa uwakilishi wa Afrika, Cape Verde imeungana na mataifa ya Morocco, Senegal, Ivory Coast, Egypt , South Africa na Ghana kufuzu hatua ya 32 bora, huku Tunisia ikiwa timu pekee kutoka Afrika iliyoaga mashindano hayo katika hatua ya makundi huku mataifa ya Algeria na Congo yakisubiri michezo Yao ya mwisho ili kujua hatima Yao.
Fahamu kuwa, Cape Verde ni taifa lenye idadi ndogo ya watu inayokadiriwa kufikia takribani 500,000, lakini wamefanya maajabu, kwa sasa taifa hilo linaendelea na safari yake katika Kombe la Dunia 2026 likiwa limeandika ukurasa mpya katika historia ya soka la nchi hiyo na kuongeza idadi ya wawakilishi wa Afrika katika hatua ya mtoano.
0767915473,
lugembetimothy01@gmail.com



Post a Comment