FEI NI MAJEREHA AU MKAKATI WA AZAM?

Timothy Lugembe,

Mwanakwetusports.

Kuondolewa kwa kiungo nyota wa Taifa Stars, Feisal Salum maarufu kama Fei Toto, katika michezo miwili ya kirafiki dhidi ya Uganda na Rwanda kumezua mjadala mkubwa miongoni mwa mashabiki wa soka nchini.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na msemaji wa Taifa Stars, Cliford Ndimbo, mchezaji huyo amewasili kambini akiwa na majeraha yaliyopelekea madaktari kumruhusu kuondoka kambini kwa ajili ya matibabu zaidi.

Hata hivyo, nyuma ya taarifa hiyo , mashabiki wengi wameanza kuhoji kama kweli ni majeraha au kuna mkakati maalum wa klabu ya Azam FC wa kumtunza nyota huyo kuelekea hatua za mwisho za Ligi Kuu Bara.

Mjadala huo umechangiwa zaidi na umuhimu mkubwa wa Feisal ndani ya kikosi cha Azam FC msimu huu. Kiungo huyo amekuwa kwenye kiwango bora akifunga mabao 14 assist 7 akiwa ndie kinara wa ufungaji pia akiwa kwenye orodha ya wachezaji bora msimu huu.

Ikiwa ligi imebakiza michezo mitano yenye ushindani mkubwa, baadhi ya wadau wanaamini Azam inaweza kuwa haitaki kuhatarisha kumpoteza mchezaji wao muhimu katika kipindi hiki nyeti cha msimu mchezaji ambaye tayari ana mchango mkubwa kwa timu yake.

Upande mwingine, wapo wanaotetea uamuzi huo wakisema afya ya mchezaji ndiyo kipaumbele kikubwa, hasa katika kipindi ambacho ratiba za soka zimekuwa ngumu na zenye msongamano mkubwa kwa wachezaji wa timu za taifa na klabu.

Mpaka sasa hakuna ushahidi wa moja kwa moja unaoonyesha kuwa Azam FC imehusika katika uamuzi huo, lakini mjadala umeendelea kushika kasi kwenye majukwaa mbalimbali ya michezo huku wengi wakisubiri kuona kama Feisal atarejea uwanjani haraka kuisaidia Azam katika mbio za mwisho wa msimu.

0767915473,

lugembetimothy01@gmail.com.


0/Post a Comment/Comments