Baada ya Kuzuiwa Kombe la Dunia, Artan Apata Heshima UEFA

  


Timothy Lugembe,

Mwanakwetusports.

Wakati mjadala kuhusu kuzuiwa kwake kuingia Marekani ukiendelea katika duru za soka, Omar Abdulkadir Artan amepata ukurasa mpya ambao umebadili mwelekeo wa simulizi yake ndani ya kipindi kifupi.

Shirikisho la Soka la Ulaya (UEFA) limemteua mwamuzi huyo kutoka Somalia kuchezesha mchezo wa UEFA Super Cup utakaowakutanisha Paris Saint-Germain dhidi Aston Villa mwezi Agosti, hatua inayokuja wiki chache baada ya kushindwa kushiriki Kombe la Dunia 2026.

Uteuzi huo umeifanya tena filimbi ya Artan kuwa sehemu ya mazungumzo ya kimataifa, huku wengi wakiendelea kufuatilia safari ya mwamuzi huyo ambaye mwaka jana alitajwa kuwa Mwamuzi Bora wa Afrika.

Awali, Artan alikuwa miongoni mwa waamuzi waliotarajiwa kusimamia michezo ya Kombe la Dunia nchini Marekani. Hata hivyo, alizuiwa kuingia nchini humo katika mazingira ambayo hayakuwekwa wazi mara moja, jambo lililomwondoa kwenye maandalizi ya mashindano hayo.

Tukio hilo liliibua maswali mengi kutoka kwa wadau wa soka, hasa kutokana na nafasi aliyokuwa ameifikia katika taaluma yake, badala ya mjadala huo kumalizika, jina lake liliendelea kutajwa katika vyombo mbalimbali vya habari na mitandao ya kijamii.

Sasa UEFA imechukua hatua ya kumpa jukumu la kusimamia moja ya mchezo utakaofungua msimu wa soka la Ulaya, ikimuweka tena kwenye jukwaa linalofuatiliwa na mamilioni ya mashabiki duniani.

Kwa Artan, uteuzi huo unakuwa fursa ya kuendelea kuonesha uwezo wake katika kiwango cha juu cha ushindani, huku kwa Somalia ukiwa mwendelezo wa uwakilishi katika medani ya soka la kimataifa.

Mchezo huo wa UEFA Super Cup utawakutanisha mabingwa wa Ligi ya Mabingwa Ulaya, Paris Saint-Germain, dhidi ya mabingwa wa UEFA Europa League, Aston Villa, ambapo macho mengi yatakuwa si kwa wachezaji pekee, bali pia kwa mwamuzi Omar Abdulkadir Artan.

0767915473,

lugembetimothy01@gmail.com.


0/Post a Comment/Comments