Timothy Lugembe,
Mwanakwetusports.
Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) imeitoza faini klabu ya Young Africans kufuatia matukio yaliyojitokeza kwenye mchezo wa Ligi Kuu ya NBC dhidi ya Simba SC uliochezwa Mei 3, 2026 katika Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo.
Kwa mujibu wa taarifa ya TPLB, Yanga imepewa onyo baada ya timu hiyo kuwasili uwanjani saa 10:35 alasiri badala ya saa 10:30 alasiri kama inavyotakiwa kwa mujibu wa kanuni za ligi kuhusu taratibu za mechi.
Mbali na onyo hilo, klabu hiyo imepigwa faini ya Sh milioni 30 baada ya wachezaji na maofisa wa ufundi kukataa kutumia chumba rasmi cha kuvalia ndani ya uwanja huo na badala yake kutumia nyumba iliyopo nje ya uwanja.
Katika hatua nyingine, Meneja wa Yanga Walter Harson amefungiwa michezo mitatu pamoja na kutozwa faini ya Sh milioni moja kwa kosa la kumsukuma mchezaji wa Simba, Clatous Chama, wakati wa mchezo huo.
TPLB pia imemfungia kuingia uwanjani kwa kipindi cha miezi 12 shabiki wa Yanga aliyetambulika kwa jina la Mohamed Ally Mposo kwa kosa la kuingia eneo la kuchezea wakati wa mapumziko na kufanya vitendo vilivyotafsiriwa kuwa ni ishara za kishirikina vilivyo husisha kumwaga maji sehemu za uwanja.
Adhabu hizo zimetolewa kufuatia kikao cha Kamati ya Uendeshaji na Usimamizi wa Ligi kilichofanyika Mei 9, 2026 kwa ajili ya kupitia matukio mbalimbali ya ligi hiyo.
0767915473,
lugembetimothy01@gmail.com.



Post a Comment