WAKONGWE WA SOKA NCHINI KUKAMILISHA UJENZI WA UWANJA NDANI YA MIEZI 20

 

Timothy Lugembe,

Mwanakwetusports.

Tangu kuanzishwa kwake mwaka 1935, ikiwa ni miaka 91 sasa, Klabu imeandika historia mbali mbali ndani na nje ya Tanzania, lakini kwa muda wote huo haikuwahi kumiliki uwanja wake binafsi, ndoto hiyo sasa inaonekana kuelekea kutimia baada ya klabu hiyo kuingia makubaliano na Kampuni ya GSM kujenga uwanja wenye umiliki wa asilimia 50 kwa 50.

Makubaliano hayo yanatajwa kuwa sehemu ya hatua mpya katika historia ya Yanga huku Mwenyekiti wa klabu hiyo, Injinia Hersi Said katika hafla hiyo ya utiaji saini ameeleza matumaini ya mradi huo kukamilika ndani ya miezi 18 hadi 20 ijayo.

“Matarajio yetu ni kwamba ujenzi wa uwanja huu utakamilika na kuzinduliwa rasmi ndani ya kipindi cha miezi 18 hadi 20 ijayo,” alisema Hersi.

Aliongeza kuwa wanaamini mradi huo utakamilika kwa wakati uliopangwa na kuwa sehemu muhimu ya historia ya klabu hiyo kongwe nchini Tanzania.

Sambamba na hayo , alitoa shukrani kwa Ghalib Said Mohamed (GSM) pamoja na familia yake kwa uamuzi walioufanya kusaidia kutimiza ndoto ya muda mrefu ya Yanga kuwa na uwanja wake.

Hatua hiyo ni funzo kwa klabu nyingine kongwe, ikiwemo Simba SC, kuharakisha mchakato wa kujenga viwanja vyao ili kupunguza utegemezi wa kuazima viwanja. Hadi sasa, baadhi ya klabu nchini tayari zimepiga hatua kwa kujenga miundombinu yao, zikiwemo Azam FC kupitia Azam Complex, KMC kupitia KMC Complex, Singida Black Stars kupitia Airtel Stadium, na Namungo kupitia Majaliwa Complex.

Hivyo vilabu kuendelea kujenga viwanja Inaonyesha kukua kwa mpira wa miguu nchini ambapo mbali na vilabu kutumia viwanja hivyo pia itatoa fursa kwa Taifa kuandaa mashindano mbali mbali ya ndani na nje kutokana na kuwepo kwa miundo mbinu ya viwanja.

0767915473,

lugembetimothy01@gmail.com.


0/Post a Comment/Comments