USHIRIKIANO WA SOKA UMEKUA KUPITIA MAANDALIZI YA PAMOJA YA MICHUANO MBALI MBALI DUNIANI

Timothy Lugembe,

Mwanakwetusports.

Mpira wa miguu ulianza kama mchezo wa kuwakutanisha watu kutoka jamii tofauti tofauti na kuwafanya kuwa kitu kimoja , Kwa muda wa dakika 90 uwanjani, mashabiki huweka pembeni tofauti zao za kijamii, kiuchumi na hata kisiasa, wakibaki na sauti moja ya kuisapoti timu wanayoipenda.

Kupitia soka, umoja na mshikamano umeendelea kujengwa miongoni mwa watu wa tamaduni mbalimbali duniani.

Kadri miaka ilivyopita, nguvu ya soka imevuka mipaka ya jamii hadi kuunganisha mataifa makubwa duniani, Mfano mkubwa ni maandalizi ya Kombe la Dunia 2026, ambapo mataifa ya Marekani, Canada na Mexico yameamua kushirikiana kwa pamoja kuandaa mashindano hayo makubwa zaidi duniani ambapo ushirikiano huo umeonyesha namna ambavyo soka linaweza kuwa daraja la kuimarisha mahusiano ya kimataifa na kuleta ukaribu kati ya nchi na nchi.

Barani Afrika pia, roho ya mshikamano kupitia soka imeendelea kuonekana kwa kasi ambapo nchi za Tanzania, Kenya na Uganda zimeungana kuandaa michuano ya AFCON 2027 katika tukio ambalo linatajwa kuwa historia mpya kwa ukanda wa Afrika Mashariki, Ushirikiano huo sio tu kwamba utaongeza maendeleo ya michezo, bali pia utafungua fursa za kiuchumi, utalii na kuimarisha undugu wa wananchi wa mataifa hayo matatu.

Cha kuvutia zaidi ni namna mataifa ya Kusini mwa Afrika nayo yalivyoamua kuonesha nguvu ya umoja kupitia mchezo huo nchi za Afrika Kusini, Zimbabwe, Botswana na Namibia zimeweka ombi la pamoja la kuandaa AFCON 2028, jambo linaloonyesha kuwa soka linaendelea kuwa chombo kikubwa cha kuunganisha mataifa, hii ni ishara kwamba mchezo wa mpira wa miguu umebadilika kutoka burudani ya kawaida na kuwa lugha ya amani, ushirikiano na maendeleo ya pamoja duniani.

Hivyo, soka limeendelea kuthibitisha kuwa zaidi ya ushindani wa uwanjani, ni nguvu inayounganisha mioyo ya watu na mataifa, Kadri dunia inavyoendelea kubadilika, mchezo huu utaendelea kuwa alama ya umoja, mshikamano na matumaini kwa vizazi vya sasa na vijavyo.

0767915473,

lugembetimothy01@gmail.com.


0/Post a Comment/Comments