Timothy Lugembe,
Mwanakwetusports.
Usiku wa Mei 30, 2026, katika dimba la Puskas Arena nchini Hungary liligeuka bahari ya maumivu huku ndoto za mamilioni ya mashabiki wa Arsenal zilivunjika mbele ya macho yao, baada ya safari ndefu ya matumaini kulisaka taji la kwanza UCL kuishia kwenye machozi na huzuni baada ya kufungwa 4-3 kwenye mikwaju ya penati kufuatia sare ya 1-1 ndani ya dakika 120 dhidi ya PSG.
Ilikuwa safari ya kipekee, Safari iliyobeba imani, subira na ndoto ya kuandika historia mpya barani Ulaya, Arsenal waliingia kwenye fainali hizo kama timu yenye njaa ya mafanikio, lakini mwisho walimaliza wakiacha simulizi ya maumivu ambayo mashabiki wao hawataisahau kwa haraka.
Katika michezo 15 waliyoicheza, Arsenal hawakupoteza hata mmoja ndani ya dakika 90 wala 120. Walishinda michezo 11 na kutoka sare mara nne, wakionyesha uimara mkubwa kuanzia hatua za mwanzo mpaka fainali.
Safu yao ya ulinzi ilikuwa ngome iliyowafanya wapinzani washindwe kupenya kirahisi huku Mfumo wa Mikel Arteta uliifanya Arsenal kuwa moja ya timu bora zaidi Ulaya msimu huu. Walicheza kwa nidhamu, kwa moyo na kwa dhamira ya kutengeneza heshima barani Ulaya.
Lakini soka lina namna yake ya kuumiza.
Usiku wa fainali, Arsenal walipambana kwa kila walichokuwa nacho, Dakika 90 zikapita bila kupatikana mshindi, Dakika 120 nazo zikamalizika huku wakiendelea kusimama imara, bado hawajafungwa ndani ya mchezo wowote katika mashindano hayo.
Mwisho wa simulizi yao haukuandikwa kwa furaha.
Mikwaju ya penati ndiyo iliyoamua hatima yao, ndani ya sekunde chache, ndoto waliyoijenga kwa miezi mingi ikayeyuka mbele ya macho yao, Wachezaji walibaki wakiwa wameinama, machozi yakitawala nyuso zao huku mashabiki wao wakishindwa kuamini kilichotokea.
Walikuwa karibu sana na historia, lakini wakabaki kuisogelea tu.
Maumivu ya kupoteza fainali hiyo hayawezi kufuta safari kubwa waliyoifanya msimu huu. Arsenal hawakumaliza mwaka wakiwa watupu, Walifanikiwa kutwaa taji la Ligi Kuu England na kuvunja ukame wa miaka 22, mafanikio yaliyowarudisha tena kwenye ramani ya timu kubwa England.
Hii inakuwa fainali ya pili kwa Arsenal kupoteza katika historia ya UCL ambapo fainali ya kwanza walicheza 2006 na kukubali kichapo Cha 2-1 dhidi ya Fc Barcelona , jambo linaloendelea kuongeza simulizi ya majaribio yao kwenye hatua ya mwisho ya mashindano hayo.
Hata hivyo, maendeleo waliyoonyesha chini ya Mikel Arteta yanaashiria kuwa klabu hiyo ipo kwenye mwelekeo sahihi wa kurejea kileleni mwa soka la Ulaya, Kwa kiwango walichoonyesha msimu huu, wengi wanaamini kuwa iwapo wataendelea kujenga kikosi chenye ushindani na kudumisha falsafa yao basi msimu ujao unaweza kuwa mwanzo wa ukurasa mpya wa mafanikio na hatimaye kutwaa taji lao la kwanza la UEFA Champions League.
0767915473,
lugembetimothy01@gmail.com




Post a Comment