SERIKALI YAANZA MAZUNGUMZO KUMLETA TYSON, MAYWEATHER TANZANIA

 

Timothy Lugembe,

Mwanakwetusports.

Serikali ya Tanzania imeanza mazungumzo ya kuwaleta mastaa wa ndondi duniani, Mike Tyson na Floyd Mayweather Jr, kwa ajili ya matukio mbalimbali ya kimichezo yatakayolenga kukuza na kuhamasisha mchezo wa masumbwi nchini.

Akizungumza Mei 1, 2026 katika hafla ya Usiku wa mapambano iliyofanyika ndani ya jengo la EACLC, Dar es Salaam, Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Paul Makonda, alisema kuwa hatua hiyo ni sehemu ya mkakati mpana wa kuinua kiwango cha mabondia wa ndani na kuitangaza Tanzania kimataifa kupitia michezo.

Makonda alifafanua kuwa mazungumzo hayo yanahusisha wadau mbalimbali wa ndondi kutoka nje ya nchi, ikiwemo viongozi wa masumbwi kutoka maeneo ya Mashariki ya Kati kama Dubai na Saudi Arabia, pamoja na ushirikiano wa karibu na viongozi wa ndondi wa ndani.


Aliongeza kuwa Serikali imejipanga kuhakikisha ujio wa nyota hao unaleta tija kwa mabondia wa Tanzania kupitia mafunzo, mapambano ya kirafiki na uwekezaji katika sekta ya masumbwi. Aidha, maandalizi yanafanyika kwa kushirikiana na waandaaji wa mapambano wa Mafia Boxing Promotion.

Hatua hiyo inatarajiwa kufungua fursa mpya kwa wanamasumbwi wa Tanzania kujifunza kutoka kwa mabingwa wakubwa duniani, huku pia ikichochea ukuaji wa sekta ya michezo na utalii wa michezo nchini.

0767815473,

lugembetimothy01@gmail.com.


0/Post a Comment/Comments