PSG WAJITWALIA UFALME ULAYA

 

Timothy Lugembe,

Mwanakwetusports.

Klabu ya Paris Saint-Germain imeendelea kuandika historia mpya barani Ulaya baada ya kutwaa taji la UEFA Champions League kwa mara ya pili mfululizo kufuatia ushindi wa penalti 4-3 dhidi ya Arsenal baada ya sare ya 1-1 ndani ya dakika 120 katika dimba la Puskas Arena nchini Hungary.

Ushindi huo umeifanya PSG kuendelea kutawala soka la Ulaya chini ya kocha wao Luis Enrique ambaye ameigeuza timu hiyo kuwa mashine ya ushindi ndani ya misimu miwili mfululizo. Mwaka 2025 waliifunga Inter Milan mabao 5-0 katika fainali, huku mwaka huu wakimaliza kazi dhidi ya Arsenal kwa changamoto ya mikwaju ya penalti.

Ubingwa huo umeifanya PSG kuingia kwenye orodha ya vilabu vilivyowahi kutwaa taji hilo mara mbili au zaidi mfululizo, orodha inayotawaliwa na Real Madrid ambao waliweka historia kwa kutwaa ubingwa huo mara nne mfululizo kuanzia 1956, 1957, 1958 hadi 1960, kabla ya kurejea tena kutwaa mataji matatu mfululizo mwaka 2016, 2017 na 2018.

Vilabu vingine vilivyowahi kutengeneza ufalme wao Ulaya ni pamoja na Benfica mwaka 1961 na 1962, Inter Milan 1964 na 1965, Ajax Amsterdam 1971, 1972 na 1973, Liverpool 1977 na 1978, Nottingham Forest 1979 na 1980 pamoja na AC Milan mwaka 1989 na 1990.


Hata hivyo kwa sasa macho yote yanaelekezwa Paris ambapo vijana wa Ufaransa wameonekana kuteka rasmi kiti cha ufalme wa soka la Ulaya baada ya kutwaa ubingwa wa Ligue 1 sambamba na UEFA Champions League ndani ya msimu mmoja.

Mbali na mafanikio ya timu, mastaa wa PSG wameendelea kung’ara mmoja baada ya mwingine huku Ousmane Dembele akiwa katika kiwango bora zaidi cha maisha yake ya soka. Nyota huyo ameendelea kuwa mhimili mkubwa wa mafanikio ya PSG, jambo linalomuweka kwenye mbio za kuwania tuzo ya Ballon d’Or baada kuchukua mwaka 2025.

Iwapo Dembele ataendelea kufanya vizuri kwenye Kombe la Dunia akiwa na timu ya taifa ya Ufaransa, nafasi yake ya kutwaa Ballon d’Or itaongezeka maradufu kama ilivyokuwa kwa baadhi ya mastaa waliotwaa tuzo hiyo baada ya kung’ara kwenye mashindano makubwa ya kimataifa.

Kwa sasa swali kubwa linalobaki ni moja tu, je PSG wataendelea kukalia kiti cha ufalme wa Ulaya msimu ujao au kutatokea mfalme mpya wa kuvunja utawala wao?

0767915473,

lugembetimothy01@gmail.com.





0/Post a Comment/Comments