PRESHA YA MASHABIKI YAMUINGIZA MKENGE ANCELLOT, NEYMAR KUUKOSA MCHEZO WA UFUNGUZI

 


Timothy Lugembe,

Mwanakwetusports.

Kocha wa timu ya taifa ya Brazil, Carlo Ancelotti, alikuwa sahihi kutomjumuisha Neymar Jr katika kikosi cha awali kuelekea Kombe la Dunia 2026 baada ya mshambuliaji huyo kupata jeraha jingine muda mfupi baada ya kurejea kwenye kikosi cha taifa.

Awali Ancelotti aliacha jina la Neymar katika kikosi cha mwanzo akieleza sababu kubwa kuwa ni kushuka kwa kiwango pamoja na kusumbuliwa na majeraha ya mara kwa mara yaliyoathiri mwendelezo wake ndani ya miaka ya karibuni.

Uamuzi huo ulizua mjadala mkubwa nchini Brazil huku mashabiki na baadhi ya wadau wa soka wakishangaa kuona nyota huyo akikosekana kwenye maandalizi ya michuano mikubwa kama Kombe la Dunia.

Kutokana na presha kubwa kutoka kwa mashabiki pamoja na Shirikisho la Soka la Brazil, Ancelotti alilazimika kumrejesha Neymar kwenye kikosi cha mwisho ili kuongeza uzoefu na nguvu katika eneo ushambuliaji ndani ya timu hiyo.

Taarifa zinaeleza kuwa nyota huyo wa Santos FC anatarajiwa kuwa nje ya uwanja kwa takriban wiki mbili hadi tatu, hali itakayo mfanya kukosa michezo miwili ya kirafiki dhidi ya Panama Mei 31, 2026, na Egypt Juni 6, 2026, na mchezo wa kwanza kombe la Dunia dhidi ya Morocco .

Jeraha hilo limekuja siku moja tu baada ya Neymar kukosa mazoezi rasmi ya kwanza ya Brazil kuelekea michuano hiyo ya FIFA, jambo lililoendelea kuongeza wasiwasi kuhusu utimamu wake wa mwili.

Matukio hayo sasa yanaonekana kuhalalisha tahadhari ya Ancelotti ya kutomtegemea Neymar mapema kutokana na historia yake ya majeraha ya mara kwa mara, licha ya ubora na mchango mkubwa aliowahi kuwa nao ndani ya timu ya taifa ya Brazil.

Hivyo, pamoja na ubora wa Neymar, Brazil kwa sasa inahitaji kujenga kikosi chenye wachezaji walio kwenye kiwango bora na wenye utimamu wa mwili ili kuongeza nafasi ya kufanya vizuri katika Kombe la Dunia 2026.

0767915473,

lugembetimothy01@gmail.com.


0/Post a Comment/Comments