“PESA NI KIRAINISHI TU, UWEKEEZAJI NI MFUMO KATIKA MICHEZO “

 

Rashid Msiri

Mwanakwetu blog

Ilikuwa ni sauti ya shabiki mmoja niliyemsikia katika kijiwe cha kahawa akipiga soga nyakati za jioni, pindi ambapo pepo za kus na kas zikivuma kwa utulivu wa hali ya juu, hali iliyonifanya ni jongee kwa upole kumsikiliza mwanakwetu huyu.

“Kuna vilabu vina pesa nyingi lakini havina utulivu, maono wala mfumo mzuri, mwisho vinaishia kushindwa. Na kuna vilabu vyenye bajeti ndogo lakini vina nidhamu, usajili sahihi, viongozi wenye maono na mashabiki wenye moyo, vinafanya vizuri sana pesa ni kirainishi tu, uwekezaji ni mfumo “ kauli hii ilinifanya nishike kalamu chini mwanakwetu na kufikiria juu ya ukweli huu mgumu kidogo .

Maisha ya michezo yamepiga hatua nyingi sana kutoka enzi ya zama za michezo ni furaha, michezo ni afya na michezo ni urafiki hadi hii leo kuwa michezo ni Ajira, yaani kiufupi ni kutoka enzi ya michezo ya ridhaa hadi hivi sasa kuwa michezo ni Ajira na sekta rasmi inayoweza kuingiza kipato kwa nchi yeyote duniani.

Dunia imekuwa ikishuhudia maelfu ya watu waliopata ajira na kufanikiwa katika uga wa kimichezo hali inayoifanya kuendelea kuwa sekta inayokuwa kwa kasi duniani kwa maana tumekuwa tukishuhudia nchi nyingi zikiongeza uwekezaji wake katika michezo, hali inayopelekea kuibuka fursa tofauti tofauti ndani ya kiwanda hicho.

Pamoja na hatua hizo kubwa za kimichezo lakini bado kumekuwepo na minong’ono mingi ambayo kila mtu amekuwa na upande wake anao uamini juu ya mafanikio chanya kwenye michezo yanahitaji fedha said au sayansi ya uendeshaji na mfumo ulio sahihi.

Ila ukweli ni kwamba Katika ulimwengu wa michezo wa kisasa, mara nyingi watu huamini kuwa fedha ndiyo kila kitu. Ni kweli pesa zina nafasi kubwa katika uendeshaji wa klabu; kuanzia usajili wa wachezaji, mishahara, usafiri, miundombinu hadi maandalizi ya timu. Lakini ukweli mkubwa ambao wengi huusahau ni kwamba mafanikio ya michezo hayajengwi na fedha pekee.

Kwani Kuna vilabu vina pesa nyingi lakini havina utulivu, maono wala mfumo mzuri, mwisho vinaishia kushindwa. Na kuna vilabu vyenye bajeti ndogo lakini vina nidhamu, usajili sahihi, viongozi wenye maono na mashabiki wenye moyo, vinafanya vizuri sana

Hii inatuonyesha ya kuwa ili mafanikio ya michezo iwepo kwa taifa husika, klabu na Jamii basi kunahitaji mfumo madhubuti wa uendeshaji wa shughuli za michezo kwa eneo husika huku kukiwa na msingi mzuri sana wa usimamizi kwa kufuata mfumo na si hisia.

Mambo ya muhimu yanayoweza kufanikisha taifa lolote kufanikiwa katika michezo au klabu ni uwepo wa;

Mfumo mzuri wa Uongozi

Mfumo mzuri wa uongozi hujengwa kwa maono, uwajibikaji na uwezo wa kufanya maamuzi sahihi kwa maslahi ya muda mrefu ya michezo. Viongozi wa kweli hawaendeshi klabu kwa mihemko ya matokeo ya mechi moja au presha za mitandaoni, bali hujenga msingi imara wa maendeleo endelevu.

Kwa ujumla, uongozi ndiyo moyo wa klabu yoyote yenye mafanikio. Wachezaji hucheza uwanjani, lakini msingi wa ushindi huanzia kwenye ofisi za viongozi. Ndiyo maana klabu nyingi kubwa duniani zimefanikiwa kwa sababu ya mifumo yao imara ya uongozi kuliko nguvu ya fedha pekee.

Maono ya muda mrefu

Klabu yenye mafanikio ya kudumu lazima iwe na maono ya muda mrefu. Katika maisha ya michezo kwa sasa, mafanikio hayawezi kujengwa kwa maamuzi ya haraka au mihemko ya muda mfupi. Maono huipa klabu dira ya kujua inapotoka, ilipo na inapotaka kwenda katika miaka ijayo.

Bila maono, klabu hujikuta ikifanya maamuzi ya kubahatisha. Leo inasajili wachezaji bila mpango, kesho inabadilisha benchi la ufundi kutokana na presha za mashabiki. Hali hii huondoa consistency na kuifanya timu ishindwe kujenga.

Nidhamu ya timu ya michezo

Nidhamu ni moja ya silaha kubwa katika mafanikio ya mpira. Timu inaweza kuwa na wachezaji wenye vipaji vikubwa, lakini bila nidhamu ni vigumu kufikia mafanikio ya kudumu. Nidhamu huanzia mazoezini, maisha binafsi ya wachezaji hadi namna timu inavyotekeleza maelekezo ya benchi la ufundi.

Benchi bora la ufundi lenye wataalamu wa kisasa

Benchi la ufundi ni ubongo wa timu yoyote ya michezo. Wachezaji huingia uwanjani kutekeleza mpango, lakini mpango huo hutengenezwa na benchi la ufundi. Ndiyo maana klabu yenye benchi bora mara nyingi huwa na uwezo mkubwa wa kufanya vizuri hata kama haina nyota wengi.

Benchi bora huhusisha wataalamu wa fitness, uchambuzi wa mechi, afya za wachezaji na maendeleo ya vipaji. Sekt ya michezo kwa sasa inahitaji taaluma na maandalizi makubwa zaidi ya kutumia vipaji pekee.

Vituo bora vya kukuza vipaji tangu awali

Academy ni moyo wa maendeleo ya muda mrefu wa klabu yoyote kubwa. Timu inayowekeza kwenye kukuza vipaji huwa na msingi imara wa mafanikio kwa miaka mingi. Badala ya kutegemea wimbi lililoibuka tu la wachezaji Kuna nyakati huwa ni ngumu kwa wataalamu kuweza kuviunganisha vipaji hivyo kutokana na kukosa utaalamu kutokea chini.

Mahusiano Mazuri Kati ya Wachezaji, Viongozi na Mashabiki

 Michezo inaounganisha watu wengi wenye malengo tofauti lakini ndoto moja. Mahusiano mazuri kati ya wachezaji, viongozi na mashabiki hujenga nguvu kubwa ya pamoja ndani ya timu.

Wachezaji wanapohisi kuthaminiwa na viongozi wao, huongeza moyo wa kujituma na kupambana kwa ajili ya timu. Vivyo hivyo, mashabiki wanapokuwa karibu na timu yao huongeza hamasa kubwa kwa wachezaji ndani na nje ya uwanja.

Licha ya yote hayo bado kuna hitajika nidhamu kubwa ya usimamizi wa mradi ili kupiga hatua kubwa katika uga wa kimichezo

Hakuna project kubwa ya mpira inayofanikiwa kwa siku moja. Mafanikio ya kweli huhitaji muda, uvumilivu na kuamini katika mchakato. Klabu nyingi hushindwa si kwa sababu ya kukosa uwezo, bali kwa kukosa subira.

Wakati mwingine timu huanza project mpya kwa kusajili kocha au kujenga mfumo mpya, lakini matokeo yasipokuja haraka presha huanza. Viongozi na mashabiki wanahitaji kuelewa kuwa maendeleo ya kweli hujengwa hatua kwa hatua.

Uvumilivu huwapa makocha na wachezaji nafasi ya kuzoea mfumo, kujenga chemistry na kuimarisha utambulisho wa timu. Bila muda wa kutosha, hata project nzuri inaweza kufa kabla haijakomaa.

Kwa ujumla, uongozi ndiyo moyo wa klabu yoyote yenye mafanikio. Wachezaji hucheza uwanjani, lakini msingi wa ushindi huanzia kwenye ofisi za viongozi. Ndiyo maana klabu nyingi kubwa duniani zimefanikiwa kwa sababu ya mifumo yao imara ya uongozi kuliko nguvu ya fedha pekee.

Mwisho wa siku, mwanakwetu fedha ni kirainishi cha maendeleo ya mpira, lakini msingi wa mafanikio ya kweli unabebwa na uongozi bora, culture ya ushindi na mshikamano wa timu.

Rashid Msiri

Whatsapp 0754645826

rashidmsiri@gmail.com


0/Post a Comment/Comments