NYOTA WA HAITI AKATAA KUCHEZA KOMBE LA DUNIA

 

Timothy Lugembe,

Mwanakwetusports.

Ukistaajabu ya Musa utayaona ya Firauni, Wakati mastaa wakubwa duniani kama Harry Maguire na Joa Pedro wakilalamikia kukosa nafasi kwenye timu zao za taifa, mshambuliaji wa RC Lens, Odsonne Edouard ameibua mjadala mkubwa baada ya kukataa kuitumikia Haiti kwenye Kombe la Dunia 2026.

Edouard ambaye ana asili ya Haiti kupitia wazazi wake, alipewa nafasi ya kujiunga na timu ya taifa hilo iliyofanikiwa kufuzu Kombe la Dunia kwa mara ya kwanza tangu mwaka 1974, hata hivyo, mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 28 amesema hajisikii kuwa sehemu ya kikosi kucheza mashindano hayo kwa sababu hakushiriki safari ya kuisaidia Haiti kufuzu.

Nyota huyo amesema hataki kuonekana kama mchezaji anayekuja dakika za mwisho kunufaika na mafanikio ya wengine bila kupitia mapambano ya awali ya timu hiyo.

Kauli hiyo imezua mijadala mikubwa katika ulimwengu wa soka, kwa upande mwingine uamuzi huo ni kuonyesha heshima, uaminifu na maadili kwa wachezaji waliopigania nafasi ya taifa hilo kufuzu hatua hiyo kubwa duniani.

Katika msimu wake, Edouard ameonyesha kiwango bora akiwa na Lens baada ya kufunga mabao 14 katika michezo 36 kwenye mashindano yote.

Timu ya taifa ya Haiti ipo Kundi C kwenye Kombe la Dunia 2026, ambapo itaanza kampeni yake dhidi ya Scotland kabla ya kucheza na Brazil na kumaliza hatua ya makundi kwa kuivaa Morocco.

0767915473,

lugembetimothy01@gmail.com.


0/Post a Comment/Comments