Timothy Lugembe,
Mwanakwetusports.
Ushindani wa kuwania tuzo ya bao bora la msimu katika Ligi Kuu ya NBC Tanzania Bara umeendelea kuchukua sura mpya huku waandaji wa tuzo hizo wanatarajiwa kuwa na kazi nzito ya kufanya maamuzi kutokana na mabao yenye ubora mkubwa yaliyofungwa msimu huu.
Kadri ligi hiyo inavyoelekea ukingoni, mabao matatu yamezua mijadala kwa mashabiki, wachambuzi na wadau wa soka nchini, wengi wakishindwa kutenganisha ubora wa kila bao kutokana na kiwango cha ufundi kilichooneshwa na wafungaji hao.
Bao la kiungo mshambuliaji wa Simba SC, Clatous Chama dhidi ya Young Africans SC limeendelea kuwa gumzo kubwa msimu huu baada ya kufungwa kwa ustadi mkubwa katika mchezo ulio wakutanisha watani wa jadi nakumalizika kwa sare ya 2-2, bao hilo lilizua mjadala mkubwa kwa wadau wengi wa soka, huku baadhi yao wakidai lina hadhi ya kuwania hata Tuzo ya Puskas duniani kutokana na ubora wake.
Wakati mjadala huo ukiendelea, mshambuliaji wa JKT Tanzania, Paul Peter naye aliingia kwenye orodha ya mabao bora baada ya kufunga bao la kuvutia dhidi ya Fountain Gate FC kwenye sare 2-2, bao hilo lilifungwa kwa ustadi kwa mtindo wa “tick tacker” kabla ya mpira kutinga wavuni, jambo lililowaacha mashabiki wengi wakisimama kushangilia ubora wa umaliziaji wake.
Aidha, beki wa TRA , Christopher Tebandeke naye ameendelea kupewa nafasi kubwa katika mbio hizo baada ya kufunga bao bora dhidi ya Mtibwa Sugar ambapo TRA walishinda 2-1, Tebandeke alitikisa nyavu kwa shuti la mbali lililopigwa karibu na eneo la katikati ya uwanja, bao ambalo limeendelea kuzungumzwa kutokana na nguvu na usahihi wake.
Kutokana na ushindani huo mkubwa, wadau wengi wa soka wanaamini kuwa mchezaji yeyote atakayeshinda tuzo hiyo atakuwa ameistahili kwa asilimia zote kutokana na ubora wa mabao yaliyoingia kwenye ushindani wa kuwania heshima hiyo msimu huu.
Ligi Kuu ya NBC Tanzania Bara ikiwa imefika mzunguko wa 24, bado wachezaji wana nafasi ya kuongeza ushindani kwa kufunga mabao mengine bora yatakayoweza kubadilisha mwelekeo wa tuzo hiyo kabla ya pazia la msimu kushushwa rasmi.
0767915473,
lugembetimothy01@gmail.com.



Post a Comment