Timothy Lugembe,
Mwanakwetusports.
WAZIRI wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Paul Makonda amemteua Haji Manara kuwa msemaji wa timu zote za taifa za Tanzania, uteuzi unaotarajiwa kuongeza nguvu katika upande wa mawasiliano, hamasa na utangazaji wa mafanikio ya timu za taifa kuelekea mashindano mbalimbali ya kimataifa.
Makonda alitangaza uteuzi huo Mei 28, 2026 jijini Dodoma ambapo alisema Manara atafanya kazi chini ya Baraza la Michezo la Taifa (BMT), akiwa na jukumu la kuimarisha taswira ya timu za taifa pamoja na kupeleka taarifa kwa wananchi kuhusu shughuli na maendeleo ya timu hizo.
Kwa mujibu wa Makonda, Manara atahusika katika ku-brand timu za taifa, kuhamasisha Watanzania kufuatilia mechi na mazoezi ya timu hizo pamoja na kuhakikisha taarifa muhimu zinawafikia wananchi kwa wakati.
Waziri huyo alisema ipo haja ya Watanzania kupewa taarifa zaidi kuhusu mafanikio ya timu za taifa ikiwemo Serengeti Boys, Taifa Stars pamoja na Tanzanite Queens ili kuongeza ushiriki wa mashabiki na kujenga uzalendo wa michezo nchini.
Uteuzi wa Manara umeonekana kuwa na mantiki kutokana na uzoefu wake mkubwa katika masuala ya mawasiliano ya michezo, hasa kipindi alipokuwa msemaji wa Simba SC na baadaye Yanga SC.
Akiwa Simba, Manara alifanikiwa kuwahamasisha mashabiki kujitokeza kwa wingi viwanjani huku akitumia mbinu mbalimbali za mawasiliano kuongeza morali ya timu hata katika nyakati ngumu. Kipindi hicho Simba ilifanya vizuri katika mashindano ya kimataifa na kufika hatua ya robo fainali mfululizo Ligi ya Mabingwa Afrika jambo lililoongeza hadhi ya klabu hiyo ndani na nje ya nchi.
Baadaye akiwa Yanga SC aliendelea kuonyesha uwezo wake wa kushawishi mashabiki na kuipa timu hamasa kubwa katika mashindano ya ndani na kimataifa, hali iliyomjengea sifa kama mmoja wa watu wenye mchango mkubwa katika upande wa utangazaji wa soka nchini.
Kupitia uzoefu wake, matarajio makubwa ni kuona viwanja vikijaa mashabiki, taarifa za timu za taifa zikisambaa kwa upana zaidi na Watanzania kuwa karibu na timu zao kuelekea mashindano yajayo ya kimataifa.
0767915473,
lugembetimothy01@gmail.com.




Post a Comment