MAMBO YAMEIVA KUELEKEA AFCON 2027, MTIFUANO KUANZA SEPTEMBA 2026

 

Timothy Lugembe,

Mwanakwetusports.

Baada ya kutangazwa rasmi kwa ratiba ya michezo ya kufuzu michuano ya AFCON 2027, mataifa ya Tanzania, Kenya na Uganda yanatarajiwa kutumia michezo hiyo kama sehemu muhimu ya maandalizi kuelekea fainali hizo ambazo zitafanyika kwa pamoja katika ukanda wa Afrika Mashariki.

Kwa mujibu wa ratiba hiyo, mechi za mzunguko wa kwanza na pili zitachezwa kati ya Septemba 21 hadi Oktoba 6 mwaka 2026, huku mizunguko ya tatu na nne ikipangwa kuchezwa Novemba 9 hadi Novemba 17 , 2026, ratiba hiyo itahitimishwa kwa michezo ya mizunguko ya tano na sita itakayochezwa Machi 22 hadi Machi 30 mwaka 2027.

Ingawa Tanzania, Kenya na Uganda tayari zimefuzu moja kwa moja kama mataifa wenyeji wa mashindano hayo, timu hizo hazitakaa pembeni katika kalenda hiyo ya CAF na badala yake, zitashiriki michezo hiyo maalum kwa lengo la kuongeza ushindani, kuimarisha vikosi vyao pamoja na kuwapa makocha nafasi ya kufanya tathmini ya mwisho kabla ya AFCON kuanza rasmi.

AFCON 2027 inatajwa kuwa ya kihistoria kwa Afrika Mashariki, huku mashabiki wakisubiri kuona namna ambavyo mataifa hayo matatu yatakavyotumia muda huu wa maandalizi kujenga timu zitakazokuwa na uwezo wa kufanya vizuri mbele ya mataifa makubwa ya Afrika.

0767915473,

lugembetimothy01@gmail.com


0/Post a Comment/Comments