LIGI KUU IMESIMAMA , MICHEZO MITANO KUAMUA HATIMA YA MSIMU

Timothy Lugembe,

Mwanakwetusports.

Ligi Kuu Tanzania Bara imeingia katika hatua ya mwisho huku ushindani ukiendelea kuongezeka kwenye mbio za ubingwa, kiatu cha ufungaji bora pamoja na tuzo ya mchezaji bora wa msimu baada ya kukamilika kwa mzunguko wa 25 leo Mei 26, 2026.

Ligi hiyo imesimama kwa muda kupisha kalenda ya FIFA na inatarajiwa kurejea Juni 12 ambapo kila timu itakuwa na michezo mitano ya mwisho kabla ya msimu kufungwa rasmi Juni 30, 2026.

Katika msimamo wa ligi, Young Africans wanaongoza kwa alama 60 huku Simba SC wakifuatia kwa alama 58, tofauti ya alama mbili pekee ikiwa imebaki michezo mitano kumalizika kwa msimu.

Mbali na mbio za ubingwa, ushindani wa kiatu cha ufungaji bora umeendelea kuwa mkali huku kiungo wa Azam fc Feisal Salum akiongoza orodha ya wafungaji akiwa na mabao 14 akifuatiwa na Allan Okello mwenye mabao 11, huku Prince Dube na Nduwumwe wakifuatia kwa mabao tisa kila mmoja.

Mbali na orodha hiyo pia kuna kundi la wachezaji sita wenye mabao 8 kila mmoja, hali inayomaanisha kuwa nafasi ya ufungaji bora bado ipo wazi kutokana na michezo mitano iliyobaki ambayo inaweza kubadilisha msimamo wa wafungaji hao.

Katika mbio za tuzo ya mchezaji bora wa msimu, ushindani umeendelea kuonekana kupitia mchango wa wachezaji kwa timu zao, Feisal Salum ameendelea kuwa kwenye hesabu baada ya kufikisha mabao 14 na assist saba, huku Allan Okello akiwa na mabao 11 na assist saba, huku Clatous Chama ameendelea kuwa miongoni mwa wachezaji wanaotajwa kwenye mbio hizo baada ya kufunga mabao nane na kutoa assist nne msimu huu.

Takwimu hizo zimeendelea kuweka wazi ushindani uliopo kuelekea mwisho wa msimu ambapo michezo mitano iliyobaki inatarajiwa kutoa majibu ya bingwa wa ligi, mfungaji bora pamoja na mchezaji bora wa msimu wa 2025/2026.

0767915473,

lugembetimothy01@gmail.com.


0/Post a Comment/Comments