ENDRICK AKATAA MWANAE KUCHEZA SOKA

 

Timothy Lugembe,

Mwanakwetusports.

Mshambuliaji chipukizi wa Real Madrid, ambaye kwa sasa yupo kwa mkopo Olympic Lyon Endrick, amesema anatamani mtoto wake wa kiume anayetarajiwa kuzaliwa hivi karibuni asifuate nyayo zake katika soka, akieleza kuwa mchezo huo una mazingira magumu na changamoto nyingi.

 Nyota huyo wa Brazil alifichua kuwa licha ya mafanikio aliyoyapata, hana hamu ya kumuona mwanaye akiingia kwenye ulimwengu wa soka. “Natumaini mwanangu atakuwa daktari, mwanasheria au kitu chochote kingine,” alisema Endrick, akisisitiza kuwa anachotamani zaidi ni mtoto wake kuwa mtu mwema na wa kipekee katika jamii.

Endrick aliongeza kuwa angependa mtoto wake amuone kama mzazi wa kawaida badala ya kumtazama kama nyota wa soka, Kauli hiyo inaonyesha mtazamo wake kuhusu maisha nje ya uwanja, akisisitiza umuhimu wa malezi na maadili kuliko umaarufu wa michezo.

Akifafanua zaidi, mshambuliaji huyo alisema soka si mazingira rahisi kama wengi wanavyodhani. “Soka si dunia rahisi, ni mazingira magumu sana,” alieleza, akigusia presha, ushindani mkali na changamoto zinazowakumba wachezaji ndani na nje ya uwanja.

Kauli ya Endrick imeibua mjadala miongoni mwa wadau wa soka duniani, wengi wakitafakari upande wa pili wa maisha ya wachezaji maarufu, hasa changamoto zinazofichika nyuma ya mafanikio yao.

0767915473,

lugembetimothy01@gmail.com.


0/Post a Comment/Comments