UCHAMBUZI WA KIUFUNDI: ATHARI ZA DABI ZANZIBAR KUELEKEA MEI 3, MEJA ISAMUHYO

 

Timothy Lugembe,

Mwanakwetusports.

Ushindi wa bao 1-0 walioupata Simba SC dhidi ya Young Africans SC katika Fainali ya kombe la muungano iliyochezwa hadi dakika 120 uwanja wa New Amaan Zanzibar umeweka msingi wa tathmini ya kitaalamu kuelekea mchezo ujao wa Mei 3, ndani ya NBC Premier League.

Kitaalamu, pambano la jana lilionyesha tofauti ya mifumo ya uchezaji kati ya timu hizo. Simba walicheza kwa nidhamu ya hali ya juu ya kujilinda, wakipunguza nafasi kati ya safu zao na kuilazimisha Yanga kucheza zaidi pembeni badala ya kupenya katikati ya uwanja, Hali hiyo ilipunguza ubora wa nafasi za kufunga kwa Yanga licha ya kumiliki mpira kwa muda mrefu katika vipindi kadhaa vya mchezo.

Kwa upande wa Yanga, walionyesha uwezo mzuri wa kujenga mashambulizi wakitumia pasi nyingi za mfululizo na kuupanua uwanja, lakini walikosa umakini katika eneo la mwisho la kufunga, Ukosefu wa maamuzi sahihi katika pasi za mwisho na umaliziaji uliwafanya washindwe kuvunja safu ya ulinzi ya Simba.

Athari kubwa kuelekea Mei 3 ipo katika vipengele vitatu muhimu, Kwanza ni uchovu wa mwili. Dakika 120 zinaongeza uchovu wa misuli na kupunguza kasi ya kurejea katika hali ya kawaida, jambo linaloweza kushusha nguvu ya mchezo ujao au kulazimisha mabadiliko ya kikosi.

Pili ni hali ya kisaikolojia , Simba wanaingia wakiwa na kujiamini baada ya ushindi, huku Yanga wakibeba presha ya matokeo ambayo inaweza kuathiri maamuzi ya haraka uwanjani, hasa katika mwanzo wa mchezo.

Tatu ni marekebisho ya mbinu, Inatarajiwa Yanga watajaribu kuongeza kasi ya mpira na kupunguza kukaa nao muda mrefu ili kuvunja uimara wa safu ya ulinzi ya Simba, huku Simba wakilenga kuimarisha zaidi mashambulizi ya kushtukiza ambayo yaliwapa faida katika mchezo uliopita.

Kwa mtazamo wa kitaalamu, dabi ya Mei 3 haitakuwa marudio bali ni mwendelezo wenye mabadiliko ya kimkakati, timu itakayofanikiwa kusimamia vyema uchovu, kufanya maamuzi sahihi katika eneo la mwisho na kubadili mbinu kulingana na mwenendo wa mchezo, ndiyo itakayokuwa na nafasi kubwa ya kuibuka na ushindi.

0767915474,

lugembetimothy01@gmail.com


0/Post a Comment/Comments