Timothy Lugembe,
Mwanakwetusports.
Klabu ya Simba imeanza kuonyesha dalili za kuyumba katika mbio za ubingwa wa Ligi Kuu NBC , baada ya kulazimishwa sare ya bila kufungana dhidi ya TRA United, katika mchezo uliopigwa Aprili 9, 2026, kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha.
Matokeo hayo yanaifanya Simba kuendelea kubaki nyuma ya wapinzani wao wa karibu Yanga, ambao wanaongoza kwa alama 44 huku Wekundu wa Msimbazi wakiwa na alama 36, huku wakiwa na mchezo mmoja mkononi na kutengeneza tofauti ya alama nane na kuwa pigo kwa matumaini ya Simba katika harakati zao za kuwania taji msimu huu.
Simba ilianza vizuri juhudi za kupunguza pengo la alama baada ya wapinzani wao kuanza kudondosha alama muhimu, hali iliyotoa matumaini kwamba wangeweza kusogea karibu zaidi kwenye msimamo wa ligi ambapo mahesabu yalifikia hadi wastani wa alama Moja iwapo mnyama angefanya vizuri kwenye michezo yake ya viporo, Hata hivyo, walishindwa kutumia ipasavyo nafasi hiyo baada ya kupoteza alama katika michezo kadhaa muhimu.
Katika mwenendo wao wa hivi karibuni, Simba walipata sare dhidi ya Pamba Jiji kabla ya kurejea kwenye ubora kwa ushindi wa michezo miwili mfululizo dhidi ya Coastal Union na TRA United. Hata hivyo, kasi hiyo haikudumu baada ya kushindwa kuibuka na ushindi katika michezo miwili iliyofuata, wakilazimishwa sare ya 0-0 dhidi ya Azam FC na kurejea tena na matokeo kama hayo dhidi ya TRA United.
Wakati huo huo, Yanga wameanza kurejea kwenye ubora wao baada ya kipindi cha sare tatu mfululizo, wakishinda michezo yao miwili iliyofuata 3-0 dhidi ya Prison na Pamba jiji na kutengeneza pengo kubwa la alama kileleni mwa msimamo.
Hali hiyo inaifanya Simba kuwa katika wakati mgumu zaidi, huku kila mchezo uliosalia ukiwa na umuhimu mkubwa kwa mustakabali wao wa ubingwa wakipaswa kuwa makini kwa kuhakikisha hawaangushi alama.
Kwa mwenendo huu, Simba wanapaswa kujipanga upya na kurejesha makali yao haraka iwezekanavyo, la sivyo ndoto yao ya kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu msimu huu inaweza kuendelea kufifia kadri muda unavyosonga mbele huku wananchi wakizidi kutwala soka la Tanzania kwa mwaka wa tano sasa.
0767915473,
lugembetimothy01@gmail.com.



Post a Comment