RUNGU BODI YA LIGI LA WAGUSA WAKUBWA WOTE

 

Timothy Lugembe,

Mwanakwetusports.

Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) imetoa maamuzi mazito ya kinidhamu kufuatia matukio mbalimbali yaliyojitokeza katika michezo ya hivi karibuni ya Ligi Kuu NBC, huku klabu kadhaa pamoja na mchezaji mmoja wakikumbana na adhabu kali katika kikao Cha April 18, 2026.

Katika mchezo namba 07 uliochezwa kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, jijini Arusha, uliomalizika kwa sare ya 0-0 kati ya TRA United na Simba SC, klabu zote mbili zimetozwa faini ya shilingi milioni tano kila moja kutokana na kosa la walinzi wao (stewards) kupigana mara baada ya mchezo kumalizika.

Kwa upande wa mchezo namba 132, ambapo Young Africans iliibuka na ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Pamba Jiji FC, kiungo Mudathir Yahya amepewa adhabu ya kufungiwa michezo mitatu pamoja na faini ya shilingi milioni moja baada ya kumpiga mchezaji wa Pamba Jiji, Ibrahim Abraham, wakati mpira ukiendelea.

Katika mchezo mwingine namba 146 uliomalizika kwa sare ya 1-1 kati ya Coastal Union na Mtibwa Sugar, klabu ya Coastal Union imepigwa faini ya shilingi milioni tano kufuatia mashabiki wake kurusha chupa za maji uwanjani, tukio lililotokea wakati wa vurugu zilizozuka kufuatia tukio la mchezaji wa Mtibwa Sugar kumsukuma mpinzani wake.

Aidha, Singida BS nao hawakupona katika mkondo huo wa adhabu baada ya kutozwa faini ya shilingi milioni tano kufuatia viongozi wao wawili kuingia uwanjani na kumwaga vimiminika, kitendo kilichotafsiriwa kama kinachochochea vurugu, katika mchezo wao dhidi ya TRA United waliopoteza kwa mabao 2-0.

Katika mchezo namba 152 uliopigwa Azam complex na kumalizika kwa sare ya 0-0 kati ya Azam FC na Simba SC, klabu ya Azam imepigwa faini ya shilingi milioni tano kwa kuruhusu baadhi ya watu kuingia uwanjani kupitia njia isiyo rasmi kinyume na taratibu za ligi.

Kwa upande wa Simba SC, wao wameadhibiwa kwa faini ya shilingi milioni kumi baada ya mashabiki wao kurusha chupa za maji kwa mwamuzi msaidizi, tukio lililotajwa kuwa ni la kujirudia ndani ya msimu huu wa 2025/2026.

Kwa ujumla, TPLB imesisitiza kuwa adhabu hizo zimetolewa kwa mujibu wa kanuni za ligi, ikiwa ni sehemu ya kuhakikisha nidhamu inazingatiwa kwa klabu, wachezaji, pamoja na mashabiki katika kuendeleza taswira chanya ya soka la Tanzania.

0757915463,

lugembetimothy01@gmail.com.


0/Post a Comment/Comments