Kariakoo Derby kupigwa Isamuhyo

Timothy Lugembe,

Mwanakwetusports.

Bodi ya Ligi Kuu Tanzania Tanzania (TPLB) , imetangaza mabadiliko ya uwanja kwa mchezo namba 169 wa Ligi Kuu ya NBC msimu wa 2025/2026, utakaowakutanisha watani wa jadi Simba SC na Young Africans SC, maarufu kama Kariakoo Derby.

Awali, pambano hilo lilipangwa kuchezwa katika Uwanja wa Benjamin Mkapa , lakini kutokana na kuendelea kwa matengenezo ya uwanja huo, mamlaka husika zimeamua kulihamishia katika Uwanja wa Meja General Isamuhyo.

Kwa mujibu wa ratiba mpya, mchezo huo utafanyika Mei 3, 2026 kuanzia saa 12:00 jioni. Mabadiliko hayo yamelenga kuhakikisha mchezo unachezwa katika mazingira salama na yenye viwango vinavyokidhi hadhi ya ligi hiyo.

Aidha, TPLB imethibitisha kuwa tayari klabu zote mbili pamoja na wadau wengine wa ligi wamejulishwa mapema kuhusu mabadiliko hayo ili kutoa nafasi ya maandalizi bora ya kiufundi na kiutawala kabla ya siku ya mchezo.

Sambamba na hilo, bodi hiyo imewataka mashabiki wa soka nchini kujitokeza kwa wingi kushuhudia pambano hilo kubwa, huku ikisisitiza umuhimu wa nidhamu na ushirikiano ili kuhakikisha mchezo unafanyika kwa utulivu.

Kariakoo Derby inaendelea kuwa moja ya michezo yenye mvuto mkubwa nchini Tanzania na ukanda wa Afrika Mashariki, hivyo matarajio ni kuona ushindani mkali na burudani ya hali ya juu kutoka kwa timu hizo mbili kongwe.

0767915473,

lugembetimothy01@gmail.com.


0/Post a Comment/Comments