Infantino: Michezo inapaswa kubaki nje ya siasa

 


Timothy Lugembe,

Mwanakwetusports.

Rais wa FIFA, Gianni Infantino, amesema kuwa michezo inapaswa kubaki nje ya masuala ya kisiasa, akisisitiza umuhimu wa mshikamano kupitia soka licha ya changamoto za kimataifa.

Akizungumza Aprili 15, 2026 katika jukwaa la CNBC Invest in America Forum, Infantino alithibitisha kuwa timu ya taifa ya Iran itashiriki Kombe la Dunia bila shaka, hata kama kuna mvutano wa kisiasa kati ya Iran na Marekani.

Kiongozi huyo alieleza kuwa matarajio ni kuona hali ya amani ikitawala ifikapo muda wa mashindano hayo, lakini akaweka wazi kuwa soka lina nafasi ya kuunganisha watu tofauti bila kujali siasa. “Iran lazima ishiriki, wanaiwakilisha nchi yao na wachezaji wanahitaji kucheza,” alisema.


Infantino pia alifichua kuwa alikutana na kikosi cha Iran wiki mbili zilizopita mjini Antalya, Uturuki, na kuvutiwa na kiwango chao cha ushindani pamoja na ari waliyonayo uwanjani.

Alisisitiza kuwa michezo inapaswa kuwa daraja la kuleta watu pamoja badala ya kuwa chanzo cha migawanyiko ya kisiasa. “Michezo inapaswa kubaki nje ya siasa,” aliongeza.

Kombe la Dunia lijalo litafanyika kwa pamoja katika nchi za Marekani, Canada na Mexico, huku Iran ikitarajiwa kucheza baadhi ya mechi zake katika majiji ya Inglewood, California na Seattle.

0767915473,

lugembetimothy01@gmail.com.


0/Post a Comment/Comments