Timothy Lugembe,
Mwanakwetusports.
Shirikisho la Soka Duniani, FIFA, limetoa tamko rasmi kuhusu hali inayoendelea katika soka la Kenya, likieleza kuwa linafuatilia kwa karibu mgogoro uliopo ndani ya federation hiyo.
Kwa mujibu wa taarifa , FIFA imesisitiza umuhimu wa kuheshimiwa kwa Katiba na taratibu za FKF, hasa katika kipindi hiki ambacho mabadiliko ya uongozi yanaendelea, Kauli hiyo inaonyesha wazi wasiwasi wa shirikisho hilo juu ya namna mgogoro huo unavyoshughulikiwa, huku likihimiza uwazi na ufuataji wa sheria za soka la kimataifa.
Pamoja na hali hiyo, FIFA bado haijachukua hatua za kinidhamu badala yake, imewataka wadau wa soka nchini humo kuhakikisha mchakato wa kutatua mgogoro unafanyika kwa haki, uwazi na kwa kuzingatia kanuni zilizowekwa.
Chanzo cha mgogoro huo kinatajwa kuwa ni tuhuma za ubadhirifu wa fedha zinazohusiana na mkataba wa bima ya mashindano ya CHAN, Kutokana na hali hiyo, baadhi ya viongozi wa FKF wamesimamishwa kupisha uchunguzi, akiwemo rais wa shirikisho hilo, Hussein Mohammed.
Kwa upande mwingine, historia ya soka la Kenya imekuwa na changamoto za mara kwa mara za kiuongozi, hali iliyowahi kusababisha vitisho vya kusimamishwa na FIFA kutokana na migogoro ya ndani pamoja na kile kinachotajwa kama kuingiliwa kwa masuala ya soka.
Katika hatua ya sasa, FIFA imeweka wazi kuwa itaendelea kufuatilia kwa makini mwenendo wa sakata hilo, Hivyo basi, mustakabali wa soka la Kenya unategemea kwa kiasi kikubwa namna wadau watakavyoshughulikia mgogoro huu kwa kuzingatia misingi ya haki na utawala bora wa michezo.
0767915473,
lugembetimothy01@gmail.com.

Post a Comment