VINICIUS NA MBAPPE WAMPIGIA CHAPUO NEYMAR TIMU YA TAIFA BRAZIL


Timothy Lugembe,

Mwanakwetusports.

WASHAMBULIAJI nyota Vinícius Junior na Kylian Mbappe wameonyesha wazi kumuunga mkono Neymar Jr kurejea katika kikosi cha timu ya taifa ya Brazil, kufuatia kuachwa kwake kwenye kikosi cha hivi karibuni kinachojiandaa na michezo ya kirafiki.

Vinícius, ambaye ni mmoja wa wachezaji tegemeo wa Brazil kwa sasa, amekiri wazi kuwa Neymar ni miongoni mwa wachezaji anaowaheshimu zaidi na anaamini bado ana mchango mkubwa ndani ya timu hiyo. Nyota huyo alisisitiza kuwa wachezaji wote wanapenda kucheza na mchezaji bora zaidi, huku akiamini Neymar bado yupo kwenye kiwango cha juu na anajitahidi kurejea katika ubora wake wa asilimia 100.

Kwa upande wake, Mbappé hakusita kueleza umuhimu wa Neymar katika michuano mikubwa kama Kombe la Dunia, akisema ni vigumu kufikiria mashindano hayo bila uwepo wa staa huyo wa Brazil. Mfaransa huyo ameongeza kuwa ana imani Neymar atakuwa fiti na tayari kushiriki michuano hiyo, akionyesha matumaini makubwa juu ya kurejea kwake uwanjani kimataifa.

Wakati wito huo ukizidi kuongezeka, presha sasa imeelekezwa kwa kocha wa Brazil, Carlo Ancelotti, ambaye anatakiwa kufanya uamuzi mgumu kuhusu mustakabali wa Neymar ndani ya kikosi hicho. Swali kubwa linalobaki ni je, ataamua kumpa nafasi staa huyo kurejea, au ataendelea na kizazi kipya kinachoijenga Brazil kuelekea mashindano yajayo?

0767915473,

lugembetimothy01@gmail.com





0/Post a Comment/Comments