RODRI AKUMBANA NA RUNGU KUTOKA FA

Timothy Lugembe,

Mwanakwetusports.

Kiungo wa klabu ya Manchester City, Rodri, ametozwa faini ya pauni 80,000 na shirikisho la mpira nchini England (FA) kufuatia kauli alizozitoa kuhusu waamuzi baada ya mchezo wa ligi uliomalizika kwa sare ya 2-2 dhidi ya Tottenham Hotspur tarehe Februari 1, 2026.

Kwa mujibu wa maelezo ya FA katika ripoti ya kesi hiyo, Rodri alikiri kosa hilo baada ya kutoa kauli zilizotafsiriwa kama kukosoa maamuzi ya waamuzi wa mchezo huo, Hata hivyo, licha ya adhabu hiyo ya kifedha, mchezaji huyo hakupokea adhabu ya kusimamishwa kucheza.

Taarifa hiyo imeeleza kuwa FA haikupendekeza adhabu ya kusimamishwa kwa Rodri, bali iliona faini ya kifedha inatosha kama onyo na hatua ya kinidhamu.

Katika barua aliyoiwasilisha kwa kamati ya nidhamu ya FA, Rodri alikubali kosa hilo huku akisisitiza kuwa hakuwa na nia ya kuathiri au kuhoji uadilifu wa waamuzi.

“Ningependa kuweka wazi kuwa sikuwa na nia ya kuashiria upendeleo wala kuhoji uadilifu wa waamuzi wa mchezo” alisema Rodri katika maelezo yake.

Adhabu hiyo ni sehemu ya juhudi za FA kudhibiti kauli zinazoweza kudhalilisha waamuzi katika soka la England.

0767915473,

lugembetimothy01@gmail.com.


0/Post a Comment/Comments