Timothy Lugembe,
Mwanakwetusports.
Mchezo wa Ligi Kuu ya NBC Tanzania Bara kati ya Simba SC na TRA United umeahirishwa kufuatia mvua kubwa iliyosababisha uwanja wa Sheikh Amri Abeid Stadium kujaa maji na kushindwa kuchezewa.
Mashabiki waliokuwa uwanjani walionyesha kutoridhishwa na uamuzi huo na kudai pesa Yao ya viingilio kurejeshwa jambo lililozua sintofahamu na kuzua vurugu huku Jeshi la Polisi likilazimika kutumia mabomu ya machozi kuwatawanya baadhi yao waliokuwa wakitaka kurejeshewa viingilio vyao.
Kwa mujibu wa Sheria ya Kwanza ya Mpira wa Miguu inayohusu uwanja na eneo la kuchezea, mchezo hauwezi kuendelea iwapo sehemu ya kuchezea haitakuwa katika hali inayoruhusu mpira kudunda au kuchezwa kwa usalama, Kutokana na mvua iliyokuwa ikiendelea kunyesha, sehemu kubwa ya uwanja ilijaa maji hali iliyofanya mpira kushindwa kudunda ipasavyo.
Kamishna wa mchezo huo wa NBC Premier League, Musa Nyamandeke, alitangaza kuahirishwa kwa pambano hilo na kueleza kuwa uamuzi huo umefikiwa kwa kuzingatia hali ya uwanja huku viongozi wa timu zote mbili wakiridhia maamuzi hayo.
Ameongeza kuwa jukumu la kupanga tarehe mpya ya mchezo huo litabaki mikononi mwa Bodi ya Ligi ambayo itatangaza siku nyingine ya kuchezwa kwa mchezo huo.
0767915473,
lugembetimothy01@gmail.com




Post a Comment