MOROCCO WAPEWA UBINGWA KWA BARUA, SENEGAL WALIA NA RUSHWA

 

Timothy Lugembe

Mwanakwetu Sports

Bodi ya rufaa ya CAF imeiondolea ubingwa timu ya taifa ya Senegal kufuatia malalamiko yaliyowasilishwa na Morocco kupinga matukio yaliyojitokeza wakati wa fainali ya AFCON 2025.

Awali, Senegal ilitangazwa mshindi baada ya kuibuka na ushindi wa bao 1-0, lakini matokeo hayo yamefutwa rasmi, CAF imeipa Morocco ushindi wa mezani wa mabao 3-0 na hivyo kutangazwa mabingwa wapya wa mashindano hayo.

Uamuzi huo umechukuliwa baada ya Senegal kukiuka kanuni za mchezo, hususan vifungu vya 82 na 84, kufuatia kitendo cha wachezaji wake kutoka uwanjani wakipinga maamuzi ya mwamuzi yaliyo onekana kuwa na utata. Timu hiyo ilikaa nje ya uwanja kwa takribani dakika kumi, hali iliyotafsiriwa kama kukiuka taratibu za mashindano.

Mshambuliaji nyota wa Senegal, Sadio Mané, ameonyesha kusikitishwa na uamuzi huo, akidai kuwa unadhoofisha maendeleo ya soka barani Afrika, Mané ameeleza kuwa maamuzi ya aina hiyo yanaweza kuvunja uhusiano kati ya soka na mashabiki wake, huku akisisitiza kuwa kuna dalili za rushwa kuathiri maamuzi hayo.

Kwa upande wake, msemaji wa serikali ya Senegal, Marie Rose Faye, amelaani vikali hatua ya kuipa Morocco ubingwa, akiitaja kuwa si ya haki, Serikali ya Senegal imetoa wito wa kufanyika kwa uchunguzi wa kina juu ya maamuzi hayo, ikihofia uwepo wa vitendo vya rushwa katika mchakato mzima.

Sakata hili linaendelea kuzua mjadala mkubwa barani Afrika, huku wadau wa soka wakitaka uwazi na haki katika maamuzi ya mashindano makubwa kama AFCON.

0767815473,

lugembetimothy01@gmail.com.


0/Post a Comment/Comments